HOTUBA YA MKUU WA WILAYA YA CHATO WAKATI WA KUTOA ELIMU YA USALAMA WA USAFIRI MAJINI WILAYANI CHATO
HOTUBA YA MKUU WA WILAYA YA CHATO KATIKA UFUNGUZI WA MKUTANO WA WADAU WA USAFIRI MAJINI WILAYANI CHATO, UKUMBI WA MKUU WA WILAYA, TAREHE 16/02/2023
Wajumbe wa Kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya,
Mkurugenzi mtendaji wa wilaya,
Maafisa wa TASAC wa Geita na Kagera,
Maafisa Uvuvi,
Wadau wa usafii na usafirishaji majini,
Wamiliki na Manahodha wa vyombo vya usafiri na Uvuvi, wasimamizi wa mialo na viongozi wa BMU,
Waandishi wa habari,
Mabibi na Mabwana,
Itifaki imezingatiwa.
Nawasalimu kwa jina la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania,
Awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema na kutuwezesha kukutana hapa kushiriki katika Mkutano wa wadau wa usafirishaji na Uvuvi katika ziwa Victoria wilayani Chato, ambao umeandaliwa na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC)
Aidha, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa namna ya kipekee kwa Mkurugenzi Mkuu, Menejimenti na Wafanyakazi wa TASAC kwa kuandaa na kuwezesha kufanyika mkutano huu wenye tija kwa Taifa na Sekta ya Usafiri Majini. Napenda pia kutoa shukrani zangu za dhati kwa Wadau wa usafiri na usafirishaji majini wilayani Chato, Wamiliki na manahodha wa vyombo vya usafiri na Uvuvi, Wajenzi wa Vyombo, Wasimamizi wa mialo, viongozi wa BMUna waandishi wa habari kwa kushiriki katika mkutano.
Ndugu Washiriki,
Naomba kabla ya yote, nichukue muda huu kueleza juu ya Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania-TASAC.
TASAC imeanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Uwakala wa Meli Tanzania Na. 14 ya mwaka 2017 na kuanza kutekeleza majukumu yake kuanzia tarehe 23 Februari, 2018 kufuatia Tangazo la Serikali (G.N. Na. 53) la tarehe 16 Februari, 2018. TASAC imeanzishwa kwa lengo la kudhibiti sekta ya Usafiri Majini ambayo awali ilikuwa ikidhibitiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA). Pia Shirika linasimamia biashara ya Huduma za Meli kwa kuthibitisha nyaraka, uondoshaji wa shehena na mizigo bandarini na uhakiki wa shehena. Shirika linasimamia pia utekelezaji wa Mikataba ya Kimataifa ya Shirika la Bahari Duniani “International Maritime Organization” (IMO) iliyoridhiwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania ni Shirika lenye jukumu la Udhibiti, Usalama, Ulinzi, Utunzaji wa Mazingira ya Bahari,Maziwa, Mito na Mabwawa pamoja na kufanya Biashara ya Meli kwa kufuata viwango vya kimataifa. Shirika lina cheti cha ubora chenye Na. ISO 9001:2015 ambacho kinatoa uhakika kwa wadau wa ndani na wa kimataifa kuwa kazi zake hufanyika kwa weledi mkubwa.
Ndugu Washiriki,
Ili kukuza uchumi wa Nchi yetu na kupata maendeleo endelevu na kwa wakati, Nawasihi kupitia Mkutano huu wa wadau wa usafiri na usafirishaji majini mkoa wa Geita na mikoa ya jirani, kufuata sheria, taratibu na kanuni za usalama wa vyombo vya majini na watumiaji wake, ambazo ni moja ya majukumu makubwa ya TASAC kupitia Kurugenzi ya Udhibiti na Usimamizi wa Usalama, Ulinzi na Utunzaji wa Mazingira majini.
Aidha napenda kutumia fursa hii kuwakumbusha kuwa katika kuimarisha usalama wa usafiri wa majini, ni wajibu wa Wamiliki na Manahodha wa (vyombo vidogo) kuzingatia yafuatayo: -
- Kuhakikisha chombo kina ubora uliostahili, kimekaguliwa na kusajiliwa na TASAC kabla yakuanza kutoa huduma Ziwani,
- Kabla ya kuanza safari, nahodha wa Kivuko (fery),boti au mtumbwi kuhakikisha kuwa boti ina vifaa vya kujiokolea vya kutosheleza, ikiwa ni pamoja na makoti ya kujiokolea,
- Kupakia abiria au mizigo kwa kuzingztia uwezo wa chombo ulioruhusiwa kubeba, na kujaza fomu ya ruhusa kutoka Bandarini au mwaloni,
- Nahodha wa chombo (kidogo) kuhakikisha watu wote walio ndani ya chombo chake, wanavaa makoti ya kujiokolea (Life jacket) muda wote wa safari,
- Kuacha taarifa za safari: chombo, abiria, mizigo na mahali kinapokwenda kwa wamiliki wa bandari/mwalo au Polisi au Ofisi ya Serikali ya eneo husika, kwa kujaza fomu za kuruhusu chombo kutoka Bandarini kabla ya kuanza safari,
- Kutoa maelekezo ya namna ya kutumia vifaa vya kujiokoa kabla ya kuanza safari,
- Kutoa taarifa kwa abiria iwapo kunatokea dharula linayosababisha chombo kusimamia safarini au kuchelewa kuanza safari,
- Kuzuia uchafuzi wa mazingira, kwa kuhakikisha kuwa boti ina vifaa vya kuhifadhi taka na taka zinawekwa katika vifaa hivyo,
- Kutoa taarifa za ajali, tukio au dharura kwa kituo cha utafutaji na uokoaji kupitia simu ya bure masaa 24 (0800110101 au 08000110107 MRCC/TASAC), kituo cha Polisi au ofisi ya Serikali,
- Kuzingatia hali ya hewa katika eneo lako na Kupata taarifa ya hali ya hewa kutoka katika mamlaka husika kabla ya kuanza safari, na kuitumia taarifa hiyo ipasavyo kwa kipindi chote cha safari ili kuepuka ajali inayoweza kusababishwa na hali mbaya ya hewa,
- Kuhakikisha chombo kinaendeshwa na idadi ya kutosha ya mabaharia wenye sifa kama ilivyoainishwa kwenye cheti cha ubora,
- Kuhakikisha chombo inaanza safari kutoka bandari rasmi au yenye usimamizi unaotambulika,
- Kuhakikisha chombo kidogo cha abiria au mizigo kinafanya safari wakati wa mchana na siyo usiku,
- Kutumia chombo/ kwa shughuli zilizoainishwa kwenye cheti cha ubora. Vyombo vya mizigo au Uvuvi visitumike kubeba abiria isipokuwa wakati wa dharura tu, na
- Kutoa tiketi kwa abiria.
Ndugu Washiriki,
Ninasisitiza wamiliki wote wa vyombo vidogo vya abiria na mizigo, na viivuko(feri) za Mv. Rubondo na Mv. Chato II hapa wilaya Chato,
- Kuwa na wafanyakazi mahiri na wenye taaluma ya ubaharia na
- Kufanyia kazi ripoti za ukaguzi wa vyombo za TASAC za kuboresha usalama wa vyombo hivyo na watumiaji wake,
Kupitia Mkutano huu mtajifunza mengi sana yenye tija kwa sisi wadau, TASAC na Taifa, hivyo basi nawasihi mtakayopata kwenye mkutano huu muyazingatie na kutoa ushrikiano wa karibu kwa TASAC. Mada mbalimbali zitawasilishwa ikiwa ni pamoja na Kanuni, Sheria na Taratibu za Shirika, katika kudhibiti na kusimamia usalama wa vyombo vya usafiri majini na utunzaji wa mazingira.
Ndugu Washiriki,
Kwa kuwa shughuli niliyoombwa kuja kutekeleza hapa ni ya kufungua rasmi mkutano huu, nisingependa kuwachosha kwa hotuba ndefu hasa ikizingatiwa uwepo wa uwasilishwaji wa mada mbalimbali, niwaombe kwa mara nyingine tena kufuatilia kwa karibu mkutano huu na mada zitakazowasilishwa kwani kila kilichoandaliwa kimeandaliwa kwa manufaa yetu, Shirika na Taifai letu kwa ujumla.
Baada ya kusema hayo, napenda sasa nitamke kuwa mkutano huu umefunguliwa rasmi niwatakie mkutano mwema na ushiriki wenye mafanikio.
Asanteni kwa kunisikiliza na ‘Kazi iendelee’
Mhe. Deusdedith Josephat Katwale,
Mkuu wa wilaya ya Chato.