Usalama, Ulinzi na Mazingira Majini

Usalama, Ulinzi na Utunzaji wa Mazingira ya Majini

Mchakato wa usajili unahusisha ufuataji wa kanuni, masharti na taratibu zilizoelezwa katika "Merchant Shipping (Registration of Ships and Licensing of Vessels) Regulations, 2005" ambazo zimeweka sifa ya kumiliki, usajili na utoaji wa leseni za meli za Tanzania. Vile vile kunahaja ya kuzingatia mikataba mbalimbali ya kimataifa inayotolewa kupitia Shirika la Bahari Duniani (IMO).

 1. Usajili na Utoaji leseni za meli;
 2. Kusimamia uajiri na ustawi wa mabaharia;
 3. Kusimamia watumishi wa vyombo vya majini, sifa na mafunzo ya mabaharia;
 4. Kushughulikia mambo ya mabaharia;
 5. Kutayarisha Kanuni za Meli za bidhaa na kuzipeleka kwa Waziri mwenye dhamana ya Meli kwa idhini na saini;
 6. Kushughulikia uzuiaji wa ajali za meli na usalama wa uongozaji meli, ikiwemo uchunguzi wa ajali;
 7. Uchunguzi na ukaguzi wa vyombo vya majini na utoaji wa hati za usalama ikiwemo:
  • Uteuzi wa wakaguzi
  • Shughuli za ukaguzi wa meli za ndani
  • Shughuli za ukazi wa Meli za nje
 8. Kupima uzito wa meli;
 9. Kuweka alama za meli kama vile, mistari ya shehena
 10. Kuhakikisha kwamba Meli zisizosalama hazifanyikazi kutokana na:
  • mitambo au vifaa visivyofaa
  • watumishi wachache
  • kuzidisha uzito, upakiaji usio salama au usio sahihi
  • mambo mengine yeyote yenye kuhusiana na usalama wa meli
 11. Kushughulikia mabaki ya meli mbovu, ikiwemo kuondoa mabaki hayo;
 12. Kusimamia mambo yanayohusu usalama wa bahari ikiwemo usalama wa vifaaa vya meli na bandari;
 13. Kusimamia mambo yanayohusu uratibu na shughuli za utafuataji na uokozi majini;
 14. Kusimamia mambo yanayohusu udhibiti wa uchafuzi wa bahari kutokana na meli;
 15. Kusimamia mambo yanayohusu usalama wa bandari; na
 16. Kuwezesha kuridhia na utekelezaji wa Mikataba mbalimbali ya Bahari

USAJILI WA MELI

Utangulizi

Mchakato wa usajili unahusisha ufuataji wa kanuni, masharti na taratibu zilizoelezwa katika "Merchant Shipping Act, 2003" ambayo imeweka sifa ya kumiliki, usajili na utoaji wa leseni za meli za Tanzania.

Hati ya Usajili

Iwapo chombo cha majini kimepotea, kimeuzwa kwa wageni au kuvunjika, notisi itolewe pamoja na Hati ya Usajili, kama ipo itumwe haraka kwa Msajili wa Meli Tanzania katika ofisi za TASAC au bandari yeyote ya usajili.

Sifa za umiliki na usajili wa meli ya Tanzania

Meli itakuwa Meli ya Tanzania kwa mujibu wa MSA, 2003 iwapo meli imesajiliwa Tanzania. Meli itakuwa imesajiliwa Tanzania kutegemea masharti mengine iwapo imemilikiwa kwa ukamilifu na watu wenyesifa ya kumiliki Meli ya Tanzania ambao ni:

 • raia wa Tanzania;
 • watu au mashirika wanaomiliki meli zilizokodiwa kwa mikataba kwa watanzania;
 • watu au mashirika yenye mikataba ya ubia kwa nia njema na Raia wa Tanzania kama itakavyoelezwa;
 • watu ambao Waziri ataamuru; na
 • Meli yoyote yenye uzito wa 50GT au zaidi inayomilikiwa na watu wenye sifa za kuwa wamiliki wa Meli ya Tanzania, watasajiliwa isipokuwa kama wamesamehewa.

Masharti ya Usajili

 • Wakati wa usajili wa meli, Msajili wa Meli atabaki na nakala moja ya cheti cha muundaji au hati ya mauzo au uthibitisho mwingine wa jina uliotolewa wakati wa usajili wa kwanza, cheti chochote cha vipimo au uchunguzi, na matamko yote ya uhalali wa kumiliki.
 • Nyaraka zozote zilizooneshwa kwa Msajili wa Meli kuthibitisha jina la mmiliki zitarudishwa kwa mwombaji mara baada ya meli kusajiliwa.

a) Jina la Chombo cha Majini

Katika kuandika jina la meli, mmiliki anaweza kupendekeza jina au majina kwa ajili ya meli yake na kuwasilisha kwa Msajili wa Meli kwa idhini. Isipokuwa kama, meli mbili au zaidi hazitakuwa na jina kwenye rejesta ya usajili.

b) Bandari ya Usajili

Mwombaji wa usajili wa meli anatakiwa achague bandari ya usajili yaani bandari maskani ya chombo chake. Bandari itakakosajiliwa meli itajulikana kuwa ni bandari ya usajili na bandari inakomilikiwa meli hiyo.

c) Cheti cha Ukaguzi na Uchunguzi

Taarifa ya ukaguzi na uchunguzi inatakiwa ili kuthibitisha kufaa kwa chombo hicho. Wakaguzi wa meli walioteuliwa kwa mujibu wa MSA, Na. 3 ya 2003 wanatakiwa kukagua na kuchunguza Meli zote za Tanzania. Uchunguzi na ukaguzi utafanywa kwenye:

 • kiunzi na mitambo;
 • zana au vifaa vya meli ikiwemo, kamba, ayari na vitu vya kuzuia kuyumba kwa meli;
 • maboya ya kujiokolea, vifaa vya zimamoto na vifaa vingine vya usalama wa meli;
 • vifaa vya mawasiliano kwa njia ya radio na simu "radiotelephony and radiotelegraphy" melini; na
 • mahali na namna ya upakiaji kwenye meli. Shehena na namna ya uwekaji shehena hatarashi.


Mabadiliko ya kutolewa taarifa

a) Mabadiliko ya jina la chombo

Mabadiliko yote ya jina la chombo ni lazima yaidhinishwe na Msajili wa Meli. Kwa hiyo, hakuna mtu atakayebadili jina la meli bila ya idhini ya Msajili wa Meli.

b) Mabadiliko ya maelezo/marekebisho

Maombi ni lazima yapelekwe kwa Msajili wa Meli kwa marekebisho yoyote yatakayoathiri usajili au kusababisha meli kusajiliwa upya.

c) Mabadiliko ya umiliki

Ili kusajili ubadilishaji wa umiliki, nyaraka zifuatazo lazima ziambatishwe na maombi ya madiliko ya umiliki:

a) Hati ya mauzo;
b) Tamko la umiliki;
c) Uteuzi wa mwakilishi aliyeidhinishwa iwapo mauzo hayo ni ya Kampuni.


Uhamisho wa meli kwa mtu asiye na sifa.

Rejesta ya usajili wa meli itafungwa iwapo chombo au hisa yoyote katika chombo inahamishiwa kwa mtu asiye na sifa au mtu asiye na sifa anapata maslahi yoyote ya pamoja katika umiliki.

Mmiliki wa meli lazima akabidhi nakala ya Hati ya Mauzo kwa Msajili wa Meli pamoja na notisi inayojumuisha maelezo ya Uraia wa mgeni na hati ya usajili ni lazima ikabidhiwe kwa Msajili wa Meli.

Ada na Tozo ya Usajili


Ada na Tozo mbalimbali hutozwa na TASAC katika ngazi mbalimbali kwa ajili ya huduma zinazotolewa kwa tasnia kama ilivyoelezwa kwenye sheria MSA Na. 3 ya 2003 na kanuni zake.