DKT. KHALID MOHAMED AKUTANA WA WAMILIKI WA MELI

Kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mabaharia Duniani, jana tarehe 24 Juni, 2025, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Dkt. Khalid Mohamed alikutana na wamiliki wa Meli na kujadili masuala mbalimbali kwa ajili ya kuboresha sekta ya usafiri majini.
Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa Mamlaka ya Usafiri Majini Zanzibar (ZMA), Dkt. Mohamed alisema kuwa Serikali inatambua mchango wa wamiliki wa meli nchini kupitia shughuli mbalimbali wanazozifanya zikiwemo uvuvi, upakiaji na upakuaji wa mizigo bandarini, uhandisi wa meli, uongozaji meli, utafutaji na uokoaji pamoja na ulinzi wa bahari yetu.
“Pamoja na mchango wenu mkubwa kutokana na shughuli mbalimbali, Serikali inatambua changamoto mnazokabiliana nazo katika kutekeleza majukumu yenu hivyo, ni imani yangu kuwa katika mkutano huu tutajadili namna bora ya kukuza sekta hii kupitia umiliki wa meli, ajira za mabaharia wa Kitanzania, na ushirikiano katika mafunzo ya vitendo kwa wahitimu wa taasisi za mafunzo ya baharini,” alisema Dkt. Mohamed.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TASAC, Naho. Mussa Mandia amewashukuru wamiliki wa vyombo kwa kushiriki katika kikao hicho na kuwakumbusha wajibu wa wamiliki pamoja na Mamlaka za Usimamizi wa Usafiri majini na wamiliki wa Meli katika kulinda na kuendeleza mazingira ya bahari kama sehemu muhimu ya maisha, ajira, biashara, na maendeleo ya kiuchumi.
Maadhimisho ya Siku ya Mabaharia Duniani yalianza rasmi tarehe 22 Juni 2025 yanafikia kilele leo tarehe 25 Juni 2025.