Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

TASAC YAKABIDHI SHILINGI BILIONI 20.45 SERIKALINI, YATUNUKIWA TUZO YA TAASISI BORA KWA UZINGATIAJI WA SHERIA

Imewekwa: 01 July, 2026
TASAC YAKABIDHI SHILINGI BILIONI 20.45 SERIKALINI, YATUNUKIWA TUZO YA TAASISI BORA KWA UZINGATIAJI WA SHERIA

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), leo Jumanne, tarehe 30 Juni 2026, limemkabidhi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, mfano wa hundi yenye thamani ya Shilingi bilioni 20.45 ikiwa ni asilimia 15 ya mapato ghafi ya Shirika kwa Mwaka wa Fedha 2025/26.

Hundi hiyo imekabidhiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya TASAC, Nahodha Mussa Mandia, pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Mohamed Salum, wakati wa hafla ya kupokea gawio na michango kutoka kwa taasisi na mashirika ya umma iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam.

Katika hafla hiyo, TASAC pia ilipata heshima ya kutunukiwa Tuzo ya Taasisi Bora kwa Uzingatiaji wa Sheria (Most Compliant Institution), ikiwa ni mwaka wa saba mfululizo kutambuliwa kwa kuzingatia misingi ya utawala bora, uwajibikaji, uzingatiaji wa sheria na utoaji wa huduma kwa viwango vinavyotakiwa.

Tuzo hiyo ilikabidhiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kupokelewa kwa niaba ya TASAC na Mwenyekiti wa Bodi, Nahodha Mussa Mandia, pamoja na Mkurugenzi Mkuu, Bw. Mohamed Salum.

Aidha, kutunukiwa tuzo hiyo sambamba na kuchangia gawio la Shilingi bilioni 20.45 kwa Serikali ni ushahidi wa mchango mkubwa wa TASAC katika kuimarisha uchumi wa taifa na utekelezaji wa malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha utawala bora, uwajibikaji, ufanisi wa taasisi za umma na usimamizi madhubuti wa rasilimali za umma.

Pichani, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya TASAC, Nahodha Mussa Mandia, na Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Mohamed Salum, mara baada ya kukabidhiwa hundi ya gawio na kutolewa kwa tuzo hiyo Ikulu, Dar es Salaam.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo