Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

WOMESA YAFANYA USAFI WA FUKWE ZA KAWE KUADHIMISHA SIKU YA BAHARI YA AFRIKA

Imewekwa: 27 July, 2026
WOMESA YAFANYA USAFI WA FUKWE ZA KAWE KUADHIMISHA SIKU YA BAHARI YA AFRIKA

Chama cha Wanawake katika Sekta ya Usafiri Majin Afrika Mashariki na Kusini (WOMESA), Tawi la Tanzania, kwa kushirikiana na wadau, tarehe 25 Julai 2026 lilifanya zoezi la usafi katika fukwe za Kawe, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Bahari ya Afrika.

Zoezi hilo lililenga kuhamasisha utunzaji wa mazingira ya bahari na matumizi endelevu ya rasilimali zake kwa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa zoezi hilo, Mgeni Rasmi, Bw. Mohamed Salum, ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) amesema ulinzi wa mazingira ya bahari ni wajibu wa kila mwananchi, kwa kuwa afya ya bahari ina uhusiano na afya ya binadamu, uchumi wa buluu na ustawi wa jamii.

Bw. Salum alieleza kuwa utupaji holela wa nyavu zilizochakaa na taka za plastiki unahatarisha viumbe wa baharini na afya za wananchi.

“Baadhi ya wavuvi wamekuwa wakichoma au kuzika nyavu zilizochakaa kandokando ya bahari. Mawimbi na upepo hurudisha mabaki ya plastiki baharini. Viumbe wa baharini wanapomeza chembe hizo huathirika, na hatimaye binadamu tunapokula samaki hao tunaweza kupata madhara ya kiafya,” amesema.

Amewataka wavuvi, kupitia Kamati za Usimamizi wa Fukwe (BMUs), kutenga maeneo maalumu ya kukusanya na kuhifadhi nyavu zilizochakaa ili zitupwe kwa njia salama.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa WOMESA Tawi la Tanzania, Bi. Fatma Masenene, alisema shirika hilo limekuwa likishirikiana na wadau kuendesha kampeni za usafi wa fukwe, kutoa elimu ya uhifadhi wa mazingira na kugawa vifaa vya usafi kwa jamii za pwani.

“Mwaka huu tumefanikiwa kufanya shughuli hizi katika fukwe za Kawe kwa ushirikiano mkubwa wa TASAC na wadau wengine,” amesema Bi. Masenene.

Siku ya Bahari ya Afrika huadhimishwa kila mwaka tarehe 25 Julai kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa bahari na kuhimiza matumizi endelevu ya rasilimali zake.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo