MABAHARIA WAHIMIZWA KUKUZA UCHUMI WA BULUU

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Bw. Makame Haji jana tarehe 24 Juni, 2025 alikutana na mabaharia kwenye warsha ya mabaharia iliyofanyika katika ukumbi wa Idrisa Abdul Wakil, Zanzibar ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Mabaharia Duniani.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Bw. Haji aliwataka mabaharia na wavuvi kutumia rasilimali za maji vizuri ili kufikia adhima ya Serikali ya kukuza uchumi wa Buluu nchini.
“Jambo kubwa ambalo limenifurahisha zaidi ni kauli mbiu ya mwaka huu: Bahari Yetu, Wajibu Wetu, Fursa Yetu inaonesha umuhimu wa mabaharia katika kukuza uchumi na heshima ya nchi yetu, kama mnavyojua nchi yetu imezungukwa na bahari, mito na maziwa, hivyo ili kuzitumia vizuri rasilimali hizo ni lazima kuwe na mabaharia pamoja na wavuvi na hatimae kufikia adhima ya Serikali ya kukuza uchumi wa Buluu,” alisema Bw. Haji.
Maadhimisho ya Siku ya Mabaharia Duniani yalianza rasmi tarehe 22 Juni 2025 na kufunguliwa na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Mhe. Dkt. Khalid Mohamed na yanatarajiwa kufikia kilele leo tarehe 25 Juni 2025 ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla.