Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

TASAC YASHIRIKI KONGAMANO LA SHULE YA SHERIA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM

Imewekwa: 08 June, 2026
TASAC YASHIRIKI KONGAMANO LA SHULE YA SHERIA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), leo tarehe 5 Juni 2026, limedhamini na kushiriki Kongamano la kila mwaka la Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSMSoL) lililofanyika katika Ukumbi wa Maktaba Mpya na kuwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya sharia nchini.

Akifungua kongamano hilo, Mhe. Ridhiwani Jakaya Kikwete (MB), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti na Utawala Bora, aliwahimiza wanafunzi kuwa waadilifu, wabunifu na kutumia ipasavyo teknolojia, hususan Akili Mnemba (Artificial Intelligence), ili kuongeza uelewa na tija katika taaluma zao na kwa taifa kwa ujumla. 

“Shule ya Sheria ya UDSM imeendelea kuzalisha wanasheria nguli ambao wanafanyakazi katika utumishi wa umma kwa kuzingatia maadili mema, huduma bora za kimahakama, haki za binadamu, sheria za kitaifa na kimataifa, utawala bora na hakuna anayeweza pinga juu ya hilo”, alisema Mhe. Ridhiwani.

Kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Wakili Judith Kakongwe, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria, ameipongeza Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kuandaa jukwaa hilo muhimu linalounganisha elimu ya sheria na utekelezaji wa taaluma kwa vitendo.

"Kama wanafunzi wa sheria, wengi wenu huenda mnaona taaluma ya sheria ikihusishwa zaidi na mahakama, mashauri ya madai na jinai, pamoja na ushauri wa kisheria. Hata hivyo, taaluma ya sheria kwa sasa imepanuka na kuvuka mipaka hiyo ya jadi,” amesema Wakili Kakomgwe.

Ameongeza kuwa TASAC inafanya kazi ndani ya sekta ya usafiri wa majini, ambayo inachangia zaidi ya asilimia 80 ya biashara ya dunia kwa ujazo wa mizigo, jambo linaloifanya kuwa eneo lenye mahitaji makubwa ya wataalamu wa sharia.

Aidha, Wakili Kakongwe alieleza kuwa taaluma ya sheria sasa inatoa fursa nyingi katika maeneo mbalimbali ikiwemo sekta ya Bahari katika Sheria ya Bahari, Sheria ya Usafirishaji na Lojistiki, Sheria ya Biashara ya Kimataifa, Bima ya Baharini, Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara, Majadiliano ya Mikataba na utekelezaji wa mikataba ya kimataifa kwa kuiingiza katika sheria za kitaifa.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo