MAKAMU WA RAIS AHIMIZA UHIFADHI WA MAZINGIRA ENDELEVU
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) leo tarehe 5 Juni, 2026 limeshiriki kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre jijini Dodoma ambapo Mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi.
Katika maadhimisho hayo, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, TASAC iliwakilishwa na Wakili Leticia Mutaki, Mkurugenzi wa Udhibiti, Ulinzi, Usalama na Utunzaji wa Mazingira ya Usafiri Majini.
Akizungumza wakati wa kufunga maadhimisho hayo, Mhe. Dkt. Nchimbi amesema Serikali itaendelea kuimarisha juhudi za uhifadhi wa mazingira nchini ili kuhakikisha Tanzania inakuwa salama dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuweka mikakati madhubuti ya kulinda mazingira sambamba na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, akionya kuwa uharibifu wa mazingira una athari kubwa kwa afya za wananchi, uchumi pamoja na ustawi wa jamii.
Ameongeza kuwa maadhimisho ya mwaka huu yamekuwa sehemu muhimu ya kuhamasisha jamii kuchukua hatua dhidi ya changamoto za taka za plastiki na uharibifu wa mazingira unaochangiwa na shughuli za kibinadamu. Amewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za uhifadhi wa mazingira ikiwemo upandaji miti, utunzaji wa vyanzo vya maji pamoja na matumizi ya nishati safi ili kupunguza athari za uchafuzi wa mazingira.
Katika maadhimisho hayo, TASAC lilishiriki kikamilifu kwa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu uhifadhi wa mazingira ya bahari, maziwa na mito pamoja na kuhamasisha uzingatiaji wa usalama na ulinzi katika shughuli za usafiri kwa njia ya maji.
Kupitia banda lake la maonesho, TASAC ilitoa taarifa na kujenga uelewa kwa wananchi kuhusu majukumu yake ya udhibiti, pamoja na kuhimiza matumizi salama ya rasilimali za maji kwa kuzingatia kanuni za utunzaji wa mazingira.
Maonesho hayo yaliyoanza rasmi tarehe 1 Juni, 2026 yamefikia kilele leo, tarehe 5 Juni, 2026, yakibeba kaulimbiu isemayo: “Dira 2050, Tuwajibike Kukijanisha Tanzania.”