Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

ZANZIBAR: TASAC YARATIBU KIKAO CHA KUKUSANYA MAONI KUHUSU KURIDHIA KIAMBATISHO CHA SITA CHA MKATABA WA KIMATAIFA WA KUZUIA UCHAFUZI WA MAZINGIRA YA BAHARI

Imewekwa: 12 March, 2025
ZANZIBAR: TASAC YARATIBU KIKAO CHA KUKUSANYA MAONI KUHUSU KURIDHIA KIAMBATISHO CHA SITA CHA MKATABA WA KIMATAIFA WA KUZUIA UCHAFUZI WA MAZINGIRA YA BAHARI

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) chini ya Wizara ya Uchukuzi, leo tarehe 12 Machi, 2025 limeratibu kikao cha wadau wa sekta ya uchukuzi majini ili kupokea maoni ya juu  ya Tanzania kuridhia Kiambatisho cha Sita cha Mkataba wa Kimataifa wa Kuzuia Uchafuzi wa Mazingira Unaotokana na Shughuli za Meli Baharini wa Mwaka 1973/1978, au kwa kifupi MARPOL ANNEX VI.

Akizungumza wakati wa kufungua kikao hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya Ardhi ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) uliopo katika Jengo la ZURA Visiwani Zanzibar, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi SMZ, Dkt. Habiba Omar amesema kuwa masuala ya udhibiti  wa uchafuzi mazingira ni suala nyeti kimataifa na kitaifa, hivyo, ni muhimu kupata maoni ya wananchi wa Zanzibar ambayo ni sehemu ya Muungano ili Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iweze kuridhia Kiambatisho hicho.

"Masuala haya ya udhibiti hapa kwetu yanahusu pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivyo maoni ya kujadili Kiambatisho hiki ni muhimu kwa Serikali ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwani Serikali zote mbili zimepiga hatua kwenye maboresho ya miundo mbinu ya usafiri majini,” amesema Dkt. Omar. 

Ameongeza kuwa kuongezeka shughuli za meli zinazokuja nchini kunaongezeka umuhimu wa kuimarisha kaguzi za meli hizo ili kulinda kulinda usalama wa mazingira hapa nchini.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Sheria TASAC, Wakili Judith Kakongwe kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TASAC amesema masuala ya usimamizi wa usafiri majini unasimamiwa na TASAC kwa Tanzania Bara na Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) kwa upande wa Zanzibar. Hivyo, suala la uridhiaji wa mikataba ya kimataifa ni la Muungano ili kuleta ufanisi katika usimamizi wake.

Wadau wameombwa kuendelea kutoa maoni kwa njia ya maandishi kupitia Wizara ya Uchukuzi na TASAC.ili kuweza kuboresha andiko hilo.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo