WATUMISHI WANAWAKE TASAC WASHIRIKI MAADHIMISHO YA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI
Watumishi wanawake wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), leo tarehe 8 Machi 2026 wameungana na wadau wa maendeleo katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika mkoani Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za kuhamasisha usawa wa kijinsia na kutambua mchango wa wanawake katika maendeleo ya taifa.
Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, ametoa wito kwa wanawake kujikita katika shughuli za kiuchumi ili kuondokana na changamoto mbalimbali ikiwemo manyanyaso wanayokumbana nayo katika jamii.
“Wanawake ni nguzo muhimu katika taifa letu. Ni muhimu wachangamkie fursa mbalimbali zilizopo, ikiwemo mikopo ya maendeleo, ili kujiimarisha kiuchumi na kuchangia maendeleo endelevu ya jamii na nchi kwa ujumla,” amesema Mhe. Chalamila.
Katika hatua nyingine, akiwasilisha risala kwa niaba ya wanawake wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bi. Suzan Kayange ameishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzisha magulio ya kila mwisho wa mwezi ili kuwapatia wanawake na wasichana fursa ya kuuza bidhaa wanazozalisha kwa mikono, hatua itakayochangia kukuza uchumi na kuongeza kipato chao.
Maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo: “Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana: Msingi Jumuishi Kufikia Dira 2050.” Kaulimbiu hiyo inalenga kuhamasisha jamii kutambua na kulinda haki za wanawake na wasichana, pamoja na kuhakikisha wanapata fursa sawa katika nyanja za maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.