Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

WADAU WA USAFIRI MAJINI MARA WASISITIZWA KUZINGATIA SHERIA KUIMARISHA USALAMA

Imewekwa: 08 March, 2026
WADAU WA USAFIRI MAJINI MARA WASISITIZWA KUZINGATIA SHERIA KUIMARISHA USALAMA

Wadau wa usafiri majini katika Mkoa wa Mara wameaswa kuzingatia kikamilifu sheria na taratibu za usafiri majini ili kuimarisha usalama wa abiria, vyombo vya majini pamoja na mazingira.

Wito huo umetolewa na Afisa Mfawidhi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC)   Mkoa wa Mara, Mha. Ezron Lusangija, wakati wa semina ya utoaji elimu kuhusu masuala ya ulinzi, usalama na utunzaji wa mazingira iliyofanyika tarehe 5 na 6 Machi, 2026 katika Kata za Kisorya na Rwamrimi mkoani humo.

Mha. Lusangija amesema kuwa ni wajibu wa kila mmiliki na mtumiaji wa chombo cha majini kuhakikisha chombo chake kinakuwa na vifaa vyote muhimu vya usalama kabla ya kuanza safari hususan jaketi okozi, pamoja na kuhakikisha vinatumika ipasavyo.

Amesisitiza kuwa wamiliki wa vyombo wanapaswa kuhakikisha boti zao zimesajiliwa rasmi na kuwa na vyeti halali vinavyotolewa na TASAC  kwa shughuli za uvuvi, usafirishaji wa abiria, mizigo au matumizi binafsi.

“Ni muhimu kwa kila anayefanya kazi katika boti kuhakikisha chombo kimesajiliwa na TASAC na kina cheti halali ambacho hakijaisha muda wake vilevile chombo kiwe na jaketi okozi za kutosha na watumiaji wazivae wakati wote wanapokuwa safarini,” alisema Mha. Lusangija.

Kwa upande wake, Bw.Magambo Josephat ambaye ni mmiliki wa boti za uvuvi akizungumza kwa niaba ya wadau wa usafiri majini, aliishukuru Serikali kwa juhudi zake za kuwajali wadau wa sekta hiyo kupitia utoaji wa elimu ya mara kwa mara kuhusu usalama majini.

“Tunashukuru TASAC kwa kuendelea kutupa elimu mara kwa mara hii inaonyesha jinsi mnavyojali maisha yetu tunaomba pia Serikali itukumbuke sisi wavuvi kwa kutupatia ruzuku ya jaketi okozi ili tuweze kupata jaketi bora kwa gharama nafuu,” alisema Bw. Magambo.

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyarusurya, Bw. Iddi Changara, amewashukuru TASAC pamoja na wadau wote waliojitokeza kushiriki semina hiyo amesisitiza umuhimu wa wadau kuendelea kushirikiana na mamlaka husika ili kuimarisha usalama majini na kuepuka visingizio vya kukosa elimu.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo