Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

WIZARA YA UCHUKUZI YAONESHA MAFANIKIO SIKU 100 ZA SERIKALI YA AWAMU YA SITA

Imewekwa: 02 February, 2026
WIZARA YA UCHUKUZI YAONESHA MAFANIKIO SIKU 100 ZA SERIKALI YA AWAMU YA SITA

Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, ametangaza mafanikio yaliyopatikana katika Wizara ya uchukuzi kwa siku 100 za Serikali ya awamu ya Sita, Kipindi cha Pili, yakihusisha reli, bandari, usafiri majini na anga.

Akizungumza Februari 1, 2026 Jijini Dodoma, Waziri Mbarawa amesema, Serikali imekamilisha taratibu za ufufuaji wa Reli ya TAZARA ambapo mkataba wa uboreshaji umesainiwa kati ya Tanzania, Zambia na Kampuni ya CCECC ya China, huku utekelezaji wa mradi ukitarajiwa kuanza Juni 2026 ili kuongeza ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam, kukuza biashara ya kikanda na ajira.

Ameeleza kuwa huduma za reli ya SGR na MGR zimeimarika, ambapo zaidi ya abiria 838,000 na tani zaidi ya 85,000 za mizigo zimesafirishwa, sambamba na Serikali kupokea vichwa viwili vya treni na mabehewa 50 ya mizigo.

Katika hatua nyingine, Shirika la Reli Tanzania (TRC) limeanza kujitegemea kifedha bila ruzuku ya mishahara, pamoja na kuanzishwa kwa Kampuni Tanzu ya TANRAIL ili kuongeza mapato na ufanisi wa reli, huku ujenzi wa reli ya SGR Dar es Salaam–Mwanza ukiendelea na kipande cha Dar es Salaam–Dodoma tayari kikitoa huduma.

Kwa upande wa bandari, Serikali imeanza maandalizi ya upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam na ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo, hatua zilizopelekea ongezeko la mapato ya TPA na TRA kwa mamia ya mabilioni ya shilingi.

Katika usafiri majini, Serikali imezindua Meli ya MV New Mwanza yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo, pamoja na kununua boti za uokoaji na Ambulance Boat kwa Ziwa Victoria.

Kwa sekta ya anga, Serikali imekamilisha ujenzi wa Jengo la Viongozi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na kuongeza vituo vipya vya kimataifa kupitia ATCL, hatua inayoongeza muunganiko wa Tanzania na masoko ya kimataifa.

Waziri amesisitiza kuwa mafanikio hayo yametokana na uongozi  mahiri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kuahidi kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya uchukuzi kwa maendeleo ya uchumi na ustawi wa Watanzania.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo