Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi SMZ afungua rasmi Maonesho ya Maadhimisho ya Siku ya Mabaharia Duniani 2024.
Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) Mhe.Dkt.Khalid Salum Mohamed amewapongeza Mabaharia kwa juhudi na uweledi katika kuhakikisha usalama wa wananchi na vyombo vya usafiri majini kwa ujumla wakati akifungua Maadhimisho ya Siku ya Mabaharia Duniani iliyofanyika Jumamosi tarehe 22 Juni,2024 wilaya ya Bagamoyo.
Hayo ameyasema wakati akiwa ni mgeni rasmi wa kufungua maonesho ya Maadhisho ya Siku ya Mabaharia Duniani.
"Wenzetu mabaharia wanafanya kazi kubwa sana. Tuna kila sababu ya kuwashukuru na kuwapongeza. Kazi ni wito na bila ninyi hali ingekuwa ngumu sana, kuongoza chombo na kukifikisha salama ni jambo kubwa mnastahili pongezi." Amesema Mhe. Dkt. Khalid
Aidha, Mhe. Dkt. Khalid amesema safari za majini zinachukua muda mrefu hivyo kuwafanya Mabaharia kukaa mbali na familia zao hivyo ni muhimu kuzingatia usalama wao mahala pa kazi kwa kuhakikisha wanasafiri na kurudi salama.
"Usalama wa Mabaharia ni kitu muhimu na lazima tuhakikishe tunaweka mazingira sawa kwanza wasafiri salama na wanapata haki zao zinazostahili. Serikali zote mbili zitafanya kila linalowezekana maslahi yenu yaendelea kuboreshwa." Amesema Mhe. Dkt. Khalid.
Maadhimisho hayo yenye Kauli mbiu ya "Mustakabali wa Uendeshaji wa Vyombo vya Usafiri Majini: Usalama Kwanza" yanatarajia kuhitimishwa tarehe 25 Juni, 2024 ambapo ndio Kilele cha Siku ya Mabaharia Duniani. Haya ni maadhimisho ya
14 ya maadhimisho ya mabaharia.