WAZIRI MKUU AFUNGA RASMI MAONESHO YA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA JIJINI DODOMA

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, ameongoza mamia ya watumishi nchini kuadhimisha kilele cha Wiki ya Utumishi wa Umma nchini, leo tarehe 23 Juni, 2025.
Akihutubia watumishi wakati wa maadhimisho hayo, amepongeza juhudi za taasisi mbalimbali za Serikali kwa kushiriki maonesho hayo yenye tija kwa watumishi wote na Watanzania kwa ujumla.
Aidha, amewasihi watumishi juu ya matumizi ya mifumo ya kidigiti yatakayosaidia urahisi wa upatikanaji wa taarifa na kuongeza ufanisi na uwajibikaji.
“Watumishi ni nguzo muhimu sana katika kukuza uchumi. Hivyo, nawasihi kufanya kazi kwa bidii na kushirikiana ili kuleta tija katika maeneo yenu ya kazi,” amesema Mhe. Majaliwa.
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) ni miongoni mwa taasisi za Serikali zilizoshiriki Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika katika viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma.
Kauli mbiu ya maonesho hayo yaliyoanza rasmi tarehe 16 Juni 2025 na kufikia kilele leo tarehe 23 Juni 2025 ni: "Himiza Matumizi ya mifumo ya Kidigiti ili Kuongeza Upatikanaji wa Taarifa na Kuchagiza Uwajibikaji.”