WADAU WAJADILI MAPENDEKEZO YA MAREKEBISHO YA ADA NA TOZO KUIMARISHA UDHIBITI WA USAFIRI MAJINI
WADAU WAJADILI MAPENDEKEZO YA MAREKEBISHO YA ADA NA TOZO KUIMARISHA UDHIBITI WA USAFIRI MAJINI
Serikali imefungua rasmi mjadala wa wadau kuhusu mapendekezo ya marekebisho ya ada na tozo za shughuli za udhibiti wa usafiri majini, hatua inayolenga kuimarisha usalama na ufanisi wa sekta bila kuongeza mzigo usio wa lazima kwa wadau.
Akifungua mkutano huo, leo tarehe 4 Machi, 2026, katika Ukumbi wa Mikutano ya Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Bw. Mabiki, ambaye ni Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Uchukuzi, amesema mapendekezo hayo yanalenga kujenga mfumo endelevu wa mapato kwa ajili ya usimamizi madhubuti wa sekta ya usafiri majini inayokua kwa kasi.
Ameongeza kuwa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) lina jukumu la kusimamia usalama, ulinzi na ufanisi wa usafiri majini, hivyo linahitaji rasilimali za kutosha ili kutekeleza majukumu yake.
Akiwasilisha mapendekezo hayo, Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Mohamed Salum, alisema mabadiliko ya kisheria yaliyofanyika mwaka 2022 kupitia Sheria ya Fedha Na. 5 ya mwaka 2022 yalipunguza kwa kiasi kikubwa shughuli za kibiashara zilizokuwa zikifanywa na Shirika hilo, hatua iliyolenga kuongeza ushiriki wa sekta binafsi katika biashara ya meli.
Bw. Salum amesema kuwa kutokana na mabadiliko hayo, mapato ya kibiashara yalishuka kwa takribani asilimia 95 kutoka Sh bilioni 39.13 hadi karibu Sh bilioni 2 kwa mwaka, hali iliyoathiri uwezo wa Shirika kugharamia majukumu ya udhibiti. Hivyo, marekebisho ya ada na tozo yatasaidia kuhakikisha huduma endelevu za usalama na ulinzi wa sekta.
Ameongeza kuwa, kwa sasa mapato ya udhibiti yanatokana na usajili wa meli, leseni za vyombo vidogo na ada za vyeti kwa mabaharia, ni takribani Shilingi bilioni 1.133 kwa mwaka kiasi ambacho hakikidhi mahitaji halisi ya utekelezaji wa majukumu ya Shirika.
Ameongeza kuwa TASAC imefanya ulinganisho na mifumo ya nchi kama Ghana na Nigeria, ambako hukusanywa tozo kupitia mizigo, ulinzi wa bahari na ada za usalama wa bandari.