MITIHANI YA MAHOJIANO KWA MAOFISA MELINI YAANZA
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) leo tarehe 2 Machi 2026, limeanza rasmi mitihani ya usaili kwa Maofisa Waongoza Meli (Deck Officer candidates) na Waandisi wa Mitambo ya Meli (Engine Room Officer candidates), ikiwa na lengo la kupata maofisa wenye leseni sahihi na utaalam wa viwango vya kimataifa katika kuongoza meli.
Akizungumza wakati wa ufunguzi kwa niaba ya Msajili na Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Mkurugenzi wa Udhibiti Uchumi, Bw. Nahson Sigalla, katika Ukumbi wa Mikutano wa TASAC, jijini Dar es Salaam, amesema kuwa Tanzania imekuwa ikipokea mrejesho chanya kutoka kwa wadau kuhusu ubora wa maofisa wa meli wenye leseni wanaozalishwa nchini.
Bw. Sigalla alibainisha kuwa TASAC inaendelea na jitihada za kusaini makubaliano ya ushirikiano (MoU) na nchi wanachama wa Shirika la Kimataifa la Bahari (IMO) pamoja na mashirika ya usalama wa bahari barani Ulaya ili kuongeza wigo wa soko la mabaharia wanaozalishwa nchini Tanzania.
“Tunatambua kuwa bado kuna changamoto katika upatikanaji wa uzoefu wa mafunzo ya vitendo baharini. Ndiyo maana tunafanya kazi ya kusaini makubaliano ya kutambuliana vyeti vya mabaharia na nchi wanachama wa IMO pamoja na mamlaka za usafiri baharini za Ulaya na barani Afrika ili kukabiliana na changamoto hizi,” alisema Bw. Sigalla.
Aidha, ameipongeza Bodi ya Mitihani (BOE) kwa mchango wake katika kusimamia mitihani ya mahojiano, kupitisha upya matokeo na kuhakikisha uendeshaji wa mitihani ya Cheti cha Umahiri (CoC) kwa mujibu wa Kanuni ya 37 ya Usafirishaji Baharini (Mafunzo, utoaji vyeti na ufanyaji kazi) ya mwaka 2016.
“Ombi langu kwenu nyote ni kuendelea kutekeleza majukumu yenu kwa bidii na uadilifu ili TASAC iwe katika viwango vya juu duniani, kama ilivyo katika dira yetu,” alisisitiza.
Jumla ya watahiniwa 60 wanashiriki katika mitihani hiyo, ambapo 23 ni wa upande wa maofisa waongoza meli (Deck Officer candidates) na 37 ni wa upande wa mitambo (Engine Room Officer cadindates). Mitihani hiyo imeanza leo tarehe 02 hadi 13 Machi, 2026.