DC NYAKIA AHIMIZA MATUMIZI YA VIFAA VYA UOKOZI ZIWA RUKWA
Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Mhe. Nyakia Ally Chirukile, amewahimiza wamiliki wa vyombo vya usafiri majini, wavuvi na wananchi wanaotumia Ziwa Rukwa kuhakikisha wanatumia vifaa okozi kila wanapoingia majini, akisisitiza kuwa usalama wa maisha ya wananchi ni kipaumbele cha Serikali.
Akizungumza wakati wa kikao kilichoandaliwa na Shirika la Uwakala la Meli Tanzania (TASAC) na kuhudhuriwa na wawakilishi wa umoja wa wavuvi wapatao 2,000 kilichofanyika mwishoni wa wiki katika eneo la Mwalo wa Msia, katika Ziwa Rukwa, Mhe. Nyakia alisema kuwa ulinzi wa maisha ya wananchi unaanza na wao wenyewe na ni kipaumbele cha Serikali, hivyo ni wajibu wa kila mtumiaji wa ziwa kuzingatia tahadhari za usalama, ikiwemo kutumia vifaa okozi ikiwemo uvaaji wa jaketi okovu na vifaa vingine vinavyokubalika kisheria.
Mhe. Nyakia alieleza kuwa baadhi ya ajali zinazotokea majini husababishwa na uzembe wa kupuuza kanuni za usalama, kupakia abiria au mizigo kupita kiasi, pamoja na kuendesha vyombo pasipo ukaguzi wa mara kwa mara. Aliongeza kuwa matumizi ya vifaa okozi si hiari bali ni wajibu kwa mujibu wa taratibu za usalama wa usafiri majini.
Aidha, aliwataka maafisa wanaosimamia usalama wa vyombo vya majini kuendelea kutoa elimu kwa wananchi, kufanya ukaguzi wa mara kwa mara, na kuchukua hatua stahiki kwa wanaokiuka sheria ili kuongeza uwajibikaji na kupunguza matukio ya ajali.
Kwa upande wake, Afisa Mfawidhi wa TASAC Mikoa ya Rukwa na Katavi, Nahodha Optatus Kalolela alieleza kuwa TASAC imekua na utaratibu wa kutoa elimu ya mara kwa mara na ufuatiliaji wa karibu ili kuhakikisha matumizi sahihi ya vifaa okozi kwa lengo la kuimarisha usalama kwa watumiaji wa Ziwa Rukwa.
Nahodha Kalolela alieleza kuwa TASAC inaendelea kutoa elimu katika mialo ya Ilanga, Msia, Nankanga na Milepa iliyo katika Ziwa Rukwa ikiwa ni utekelezaji wa mikakati ya uhamasishaji wa elimu ya usalama wa usafiri majini katika maziwa na maeneo ya bahari nchini, kwa lengo la kulinda maisha na mali za wananchi wanaotegemea usafiri wa majini kwa shughuli zao za kila siku.