WANAWAKE WAPONGEZWA KWA MCHANGO WAO KATIKA MAENDELEO YA SEKTA YA USAFIRI MAJINI
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) ambaye pia ni Mkaguzi Mkuu wa Ndani, CPA. Mwatano Maganga, amewapongeza wanawake wanaofanya kazi katika sekta ya usafiri majini kwa mchango wao mkubwa katika kuendeleza uchumi wa buluu na kuimarisha huduma za usafiri majini nchini.
CPA. Maganga ametoa pongezi hizo leo, Mei 18, 2026, wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake katika Sekta ya Usafiri Majini yaliyofanyika katika Ukumbi wa Oceanic Bay, Bagamoyo, mkoani Pwani, ambapo alikuwa mgeni rasmi.
“Tunajivunia wanawake waliopo katika sekta ya bahari kwa kazi kubwa na ya mfano wanayoendelea kuifanya kama manahodha, wahandisi wa meli, wasimamizi wa bandari pamoja na wataalamu wa kada mbalimbali zinazochochea maendeleo ya sekta ya usafiri majini nchini. Wanawake hawa wameendelea kuonyesha uwezo mkubwa, weledi wa hali ya juu na uzalendo katika kuhakikisha sekta ya bahari inakuwa salama, yenye ufanisi na yenye mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa taifa,” amesema CPA. Maganga.
Aidha, amesema ameridhishwa na kazi kubwa inayofanywa na Umoja wa Wanawake wanaofanya kazi katika Sekta ya Bahari katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini (WOMESA) katika kuhakikisha wanawake wanapata nafasi na fursa zaidi ndani ya sekta hiyo muhimu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa WOMESA Tanzania, Bi. Fatuma Masenene, amesema kuwa uwepo wa WOMESA umeendelea kuwa chachu ya maendeleo na kuhamasisha usawa wa kijinsia katika sekta ya usafiri majini.
“Lengo letu ni kuona wanawake wengi zaidi wakishiriki na kufanikiwa katika sekta ya bahari kupitia uwezeshaji, mafunzo na ushirikiano wa wadau mbalimbali,” amesema Bi. Masenene.
Katika hatua nyingine, Bi. Masenene amewashukuru wadhamini, washiriki na wageni wote waliohudhuria maadhimisho hayo kwa mchango wao mkubwa uliofanikisha tukio hilo muhimu kwa wanawake wa sekta ya bahari nchini.