Wanafunzi wa JWTZ wafanya ziara ya mafunzo TASAC
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala Meli Tanzania (TASAC), Bw. Mohamed Salum amepokea ugeni wa wanafunzi wa ubaharia kutoka Shule ya Ubaharia ya Jeshi (JWTZ) Kamandi ya Wanamaji, tarehe 16/07/2024 kwenye ofisi za TASAC jijini Dar Es salaam. Ziara hiyo imelenga kuzungumzia masuala mbalimbali yanayohusiana na utendaji wa Kituo cha Utafutaji na Uratibu wa Uokoaji cha Dar es salaam.
Bw. Mohamed ameshukuru wanafunzi hao kwa kuichagua TASAC kuja kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo jinsi Kituo cha Utafutaji na Uratibu wa Uokoaji cha Dar es salaam kinavyohudumia wananchi.
" Tunashukuru kuja kwenu na naomba tuendelee kushirikiana kwenye majukumu ya kuwahudumia wananchi kwa usafiri salama na bora", amesema Bw. Mohamed.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Usalama, Ulinzi na Utunzaji mazingira majini, Bw. Lameck Sondo amesema ni muhimu kupashana habari ili kudhibiti huduma za usafiri majini.
"Tuna maeneo muhimu ya ushirikiano ya kuwasiliana kuhusiana na shughuli za meli zinazofanywa maeneo yetu ya maji maana meli inaunganisha nchi na nchi na bandari inaunganisha nchi na nchi", amesema Bw. Sondo.
Aidha, Sajini taji Swahibu Kabende kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania alishukuru TASAC kuendelea kuweka milango wazi na kuendelea kushirikiana katika kudhibiti matumizi mazuri ya maeneo ya maji yetu.
"Tumeichagua TASAC na kuwaleta askari wanafunzi wa ubaharia kuja kujifunza vema jinsi mamlaka hii inavyotekeleza majukumu ya utafutaji na kuratibu uokoaji majini pale ajali inapotokea". Amesema Sajini taji Swahibu.
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na TASAC wameendelea kujenga mahusiano ya karibu ya kupashana habari na uzoefu.
Askari mwanafunzi Ismail Namahara amesema wamejifunza mengi na kuona kumbe raia wanaweza kuwasaidia kuwapa taarifa zitakazosaidia kulinda rasmali za nchi.
Ugeni huo umetembelea Kituo cha Utafutaji na Uratibu wa Uokoaji cha Dar es salaam kujifunza kwa vitendo.Hii ni ziara ya tatu ya Jeshi kutembelea TASAC tangu mwaka huu uanze.