Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

WAKILI MUTAKI: MABAHARIA LAZIMA KUWA NA NDOTO KUBWA ILI KUENDANA NA KASI YA UKUAJI WA SEKTA YA BAHARI DUNIANI

Imewekwa: 23 October, 2025
WAKILI MUTAKI: MABAHARIA LAZIMA KUWA NA NDOTO KUBWA ILI KUENDANA NA KASI YA UKUAJI WA SEKTA YA BAHARI DUNIANI

Mkurugenzi wa Udhibiti Usalama, Ulinzi wa Vyombo vya Usafiri Majini na Utunzaji wa Mazingira wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Wakili Leticia Mutaki ametoa wito kwa mabaharia nchini kujiendeleza kielimu na kitaaluma ili kuongeza maarifa na weledi utakaoiwezesha Tanzania kuwa kitovu cha usafirishaji majini duniani.

Wito huo umetolewa leo tarehe 23 Oktoba, 2025 wakati wa Kikao Kazi cha Kurugenzi ya Usalama, Ulinzi wa Vyombo vya Usafiri Majini na Utunzaji wa Mazingira Majini (DMSE), kinachofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere mjini Kibaha.

Akizungumza katika kikao hicho, Wakili Mutaki amesema kuwa mafanikio makubwa katika sekta ya usafiri majini hayaji kwa bahati bali kupitia ndoto kubwa, maono sahihi na utekelezaji wa mikakati thabiti.

“Baharia anatakiwa kuota ndoto kubwa ya mafanikio kupitia kujiendeleza kielimu ili iwe chanzo cha msukumo wa kupanga na kuweka mikakati itakayowezesha maendeleo makubwa ya sekta ya usafiri majini, yenye manufaa kwa uchumi wa taifa,” amesema Wakili Mutaki.

Kwa upande wake, Meneja wa Mipango na Ufuatiliaji wa TASAC, Bw. Makiri Ngangaji, amewahimiza mabaharia kujikita katika fikra bunifu na kushiriki kikamilifu katika kutoa maoni yatakayosaidia kuboresha mipango na mikakati ya taasisi hiyo.

“Tukijikita kwenye mawazo chanya na ushirikiano, tunaweza kuipeleka Tanzania katika hatua ya kuwa kitovu cha usafiri wa majini Afrika na duniani. Ushiriki wenu ni muhimu katika kuboresha dira na malengo ya TASAC,” aliongeza Bw. Ngangaji.

Kikao kazi hicho kimejumuisha majadiliano kuhusu mipango, bajeti na miongozo ya kitaifa na kimataifa, ikiwemo mikakati ya kuimarisha usalama baharini, ulinzi wa mazingira, na ustawi wa mabaharia pamoja na kuboresha utendaji kazi wa watumishi na kuhakikisha huduma zote za baharini zinafuata viwango vya kimataifa vilivyowekwa na mashirika kama IMO (International Maritime Organization).

Mrejesho, Malalamiko au Wazo