Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

WADAU WAWEKA MIKAKATI IMARA UTEKELEZAJI WA MFUMO WA DIRISHA MOJA

Imewekwa: 16 April, 2026
WADAU WAWEKA MIKAKATI IMARA UTEKELEZAJI WA MFUMO WA DIRISHA MOJA

Wadau wa sekta ya usafiri kwa njia ya maji wameweka mikakati madhubuti ya kuimarisha utekelezaji wa Mfumo wa Dirisha Moja la Huduma za Usafiri kwa Njia ya Maji (Maritime Single Window – MSW), ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mafunzo ya kikanda yatakayofanyika kuanzia Aprili 20 hadi 24, 2026 katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Katika kikao hicho, wadau walijadili kwa kina changamoto zilizopo pamoja na kubaini maeneo yanayohitaji maboresho ili kuhakikisha mfumo huo unatekelezwa kwa ufanisi na kuleta matokeo chanya katika sekta ya usafiri majini.

Akifungua kikao hicho, Mkurugenzi wa Udhibiti wa Huduma za Meli kutoka Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Bw. Nelson Mlali, amewataka wadau kutumia fursa hiyo kujadili changamoto zilizopo na kubuni suluhisho la pamoja litakaloboresha utekelezaji wa majukumu katika mzunguko mzima wa huduma za meli.

Bw. Mlali amesema kuwa hatua hizo zitasaidia kuimarisha mfumo wa MSW na kuhakikisha unaendana na viwango vya kimataifa vilivyowekwa na Shirika la Bahari Duniani (IMO), pamoja na kuongeza ufanisi na uwazi katika sekta ya usafiri kwa njia ya maji.

Mfumo huo unatarajiwa kurahisisha michakato ya utoaji huduma kwa kuunganisha taasisi zote muhimu katika dirisha moja la kidijitali, hatua itakayopunguza urasimu, kuongeza kasi ya huduma na kuvutia meli nyingi zaidi kutumia bandari za Tanzania.  

Kikao hicho kiliwakutanisha wadau mbalimbali kutoka sekta ya umma na binafsi katika usafiri kwa njia ya maji, wakiwemo Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) ambao ni wadhibiti wa huduma za Usafiri kwa njia ya maji,  Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Idara ya Uhamiaji, Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),  Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA), Mamlaka ya Serikali Mtandao Zanzibar, Wizara ya Afya kupitia Kitengo cha Afya Bandarini (Port Health), Shirika la Viwango Tanzania, pamoja na mawakala wa meli.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo