Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

WADAU WATOA MAONI TOZO ZA HUDUMA BANDARI YA DAR ES SALAAM

Imewekwa: 14 February, 2025
WADAU WATOA MAONI TOZO ZA HUDUMA BANDARI YA DAR ES SALAAM

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), leo tarehe 13 Februari 2025 limekutana na wadau mbalimbali wanaotoa huduma katika Bandari ya Dar es Salaam kukusanya maoni kuhusu kuwianisha tozo za huduma katika bandari hiyo katika kikao kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwl. Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa kufungua mkutano huo, Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Mohamed Salum amesema mkutano unafanyika kwa mujibu wa kifungu cha 29 cha Sheria ya Uwakala wa Meli Tanzania, Sura ya 415, ukiwa na lengo la kuwashirikisha wadau katika kukusanya maoni ili kutatua changamoto ya tofauti za ushuru kati ya watoa huduma binafsi katika Bandari ya Dar es Salaam ambao ni DP World na Tanzania East Africa Gateway Terminal Limited (TEAGL). 

“Shirika linafahamu tofauti za tozo zilizopo kati ya watoa huduma binafsi za kibandari katika bandari ya Dar es Salaam na hii imepelekea kuwa na changamoto mbalimbali ikiwemo tozo zisizo na uwiano kwa wateja wanaotumia bandari; uwepo wa muundo wa tozo za Bandari usio rafiki kwa watumiaji na hamasa duni kwa waendeshaji wa bandari kushindana na kuboresha ubora wa huduma,” amesema Bw. Salum.

Ameongeza kuwa mkutano huo ni muhimu katika mchakato mzima wa ukaguzi wa ushuru kwa huduma zinazodhibitiwa na TASAC na kuwashauri wadau kutoa maoni yao kwa uwazi.

Akiwasilisha wasilisho la uwianishaji wa tozo za huduma katika Bandari ya Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Udhibiti Uchumi TASAC, Bw. Nahson Sigalla amesema kuwa ili kutatua changamoto zilizopo katika Bandari ya Dar es Salaam ni muhimu kuchambua tofauti za tozo zilizopo kati ya watoa huduma na kuwianisha tozo za utunzaji wa makasha zinazotolewa na waendeshaji wawili bandarini hapo.

Aidha amewaasa wadau kutumia fursa ya mkutano huo kutoa maoni kwa uwazi lakini pia kuendelea kutoa maoni kupitia maandishi kabla ya tarehe 21 Februari 2025.

Wadau takribani miamoja (100) wanaojishughulisha na huduma katika bandari ya Dar es Salaam wamekutana kujadili tozo hizo ikiwemo Wizara ya Uchukuzi, TPA, TBS, DP World, TEAGL, CIDAT, CALAT, SEAFORTH, PIL (T) na CENTRAL CORRIDOR.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo