WADAU WATAKIWA KUSHIRIKIANA KUONGEZA MAPATO YA SERIKALI

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mhe. Meja Edward Gowele, amehimiza taasisi za Serikali, binafsi na Wakala wa Forodha kufuata taratibu za leseni na kushirikiana kwa pamoja katika utoaji huduma za kiforodha ili kuongeza mapato ya Serikali na kuinua uchumi wa Taifa.
Ameyasema hayo, leo, tarehe 14 Desemba, 2024, wakati akiendesha kikao cha wadau kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kituo cha Pamoja cha Forodha cha Mpaka wa Sirari, wilayani Tarime, mkoa wa Mara.
Kikao hicho kiliwakutanisha wamiliki wa kampuni binafsi za uwakala wa forodha, Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Mamlaka ya Usimamizi wa Mapato Tanzania (TRA), taasisi na mamlaka mbalimbali za Serikali zinaohusika katika mnyororo wa kusafirisha shehena kwa njia ya maji kupitia katika mpaka wa Sirari.
"Kikao hiki kinalenga kuboresha utoaji wa huduma za kiforodha katika Kituo cha Mpaka wa Sirari ambacho kinahudumia mataifa yanayopitisha mizigo yao kwenye bandari zetu au za nchi jirani," amesema Mhe. Gowele.
Ameongeza kuwa, kila mdau anapaswa kuwa na ofisi maalum kama inavyotakiwa na sheria, pia kila wakala wa forodha kutambulika wakati anatoa huduma kwa kuvaa kitambulisho.
"Ni ukweli usiopingika kuwa Serikali inafanya kazi na sekta binafsi ila inabidi kuvaa sare na vitambulisho vinavyotambulika", ameongeza.
Kikao hiki kimeratibiwa na TASAC ambapo wametumia fursa hiyo kutoa elimu ya majukumu wanayotekeleza katika kusimamia huduma za uwakala wa forodha.
Akizungumza katika kikao hiko, Mtakwimu Mwandamizi wa TASAC, Bw. Athman Athman amesema sekta ya usafiri majini ni nguzo muhimu katika uchumi, hivyo, watoa huduma wanatakiwa kuwa waadilifu katika kufuata masharti ya leseni.
"Mawakala wote wanahitaji kuwa na ofisi ya kutoa huduma na wawe na leseni ya TASAC," amesema Bw. Athman.
Mmoja wa Watoa Huduma ya Forodha Mpakani hapo, Bi Maryam Muhambo amesema kuna baadhi ya mawakala wa forodha wachache wanakaidi mamlaka za Serikali.
Mhe. Gowele alihitimisha kikao hicho kwa kuwaelekeza TASAC, TRA na TAFFA kuendelea kutoa elimu ya namna bora ya kutoa huduma ya forodha.