WADAU KAGERA WATOA MAONI MAOMBI YA NAULI ZA MV NEW MWANZA
Wadau wa usafiri kwa njia ya maji mkoani Kagera, leo tarehe 19 Novemba, 2025 wametoa maoni na mapendekezo yao kuhusu maombi ya nauli za abiria na mizigo kwa meli ya MV New Mwanza, katika kikao cha pili cha wadau kilichoandaliwa na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC).
Kikao hicho kilifanyika katika Manispaa ya Bukoba na kilifunguliwa rasmi na Mkuu wa Wilaya ya Misenyi, Kanali Mstaafu Hamis Mayamba Maiga, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kagera.
Katika hotuba yake, alisisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa wananchi katika maamuzi yanayogusa huduma za kijamii, hususan usafiri wa majini unaotegemewa na wakazi wa ukanda wa Ziwa Victoria.
Akizungumza katika kikao hicho kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Nahson Sigalla aliwahimiza wadau kuendelea kuwasilisha maoni yao kupitia ofisi za TASAC zilizopo mkoani Kagera.
“Lengo la kikao hiki ni kukusanya maoni ya wadau na wananchi kabla ya kuanza kutumika kwa nauli zinazopendekezwa, baada ya Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO) kuwasilisha maombi ya nauli kwa ajili ya meli ya MV New Mwanza,” amesema Bw. Sigalla.
Wakizungumza katika kikao hicho, wadau walipongeza ujio wa meli hiyo, wakieleza kuwa itaongeza fursa za kiuchumi, kuboresha usafiri wa abiria na mizigo, pamoja na kuchochea biashara kati ya mikoa inayozunguka Ziwa Victoria. Hata hivyo, walitoa maoni mbalimbali wakisisitiza umuhimu wa nauli kuwa rafiki kwa wananchi wa kipato cha chini, wavuvi, wafanyabiashara wadogo na wanafunzi.
Bw. Sigalla aliwaeleza wadau kuwa maoni yaliyotolewa yatafanyiwa kazi kwa mujibu wa sheria na kanuni za udhibiti wa huduma za usafiri majini, kabla ya kufanyika kwa maamuzi ya mwisho kuhusu viwango vya nauli za MV New Mwanza.
Bw. Sigalla ameongeza kuwa TASAC inaendelea kukusanya na kuchambua maoni ya wadau kwa ajili ya kufanya tathmini ya kina kabla ya kutoa mapendekezo ya mwisho kuhusu nauli husika. Maoni ya wadau yataendelea kupokelewa hadi tarehe 30 Desemba, 2025.