UTEKELEZAJI IOMOU WASAIDIA ONGEZEKO LA UKAGUZI WA MELI ZA KIGENI
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu, Mawasiliano na Uchukuzi – Zanzibar, Bw. Makame Haji amesema Tanzania kama nchi mwanachama wa Hati ya Makubaliano ya Ukaguzi wa Meli katika ukanda wa Bahari ya Hindi (IOMOU) imefanikiwa kutatua changamoto mbalimbali zilizokuwa zinakwamisha utekelezaji wa IOMOU.
Akizungumza wakati wa kufunga Mkutano wa 27 wa IOMOU katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Bw. Haji amesema kuwa Tanzania imechukua hatua kubwa katika kuhakikisha inatekeleza kwa ufanisi Hati ya Makubaliano kwa kutatua changamoto hizo ikiwemo ukaguzi wa meli za kigeni zinazoingia bandarini.
“Sisi, Tanzania tumechukua juhudi kubwa, hapo awali kulikuwa na changamoto lakini kwa sasa tumefanya vizuri tumeweza kuongeza idadi ya kaguzi za meli za kigeni zinazoingia nchini. Kwa mwaka 2023 kama ilivyoelezwa katika Mkutano huu matokeo yetu yamekuwa mazuri zaidi ukilinganisha na miaka minne iliyopita na tumeweza kukagua vyombo 355,” amesema Bw. Haji.
Aidha ameongeza kuwa, Tanzania imeweza kutatua changamoto ya wataalam wa kukagua meli kwa kutenga fedha na kuwapa mafunzo watumishi ili kuwawezesha kufanya kaguzi.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Bw. Nahson Sigalla amesema lengo la Mkutano huu ni kuwa na mikakati ya pamoja ili kuimarisha usalama wa vyombo vinavyokuja katika bandari zilizo katika nchi wanachama wa Hati ya Makubaliano, kulinda mazingira pamoja na kulinda mali zinazobebwa na vyombo hivyo ili kuchoche Uchumi.
Mkutano wa 27 wa IOMOU, ulifunguliwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Kahyarara, tarehe 26 Agosti, 2024 na umefungwa leo tarehe 30 Agosti, 2024 na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Miundombinu, Mawasiliano na Uchukuzi - Zanzibar Bw. Makame Haji katika Ukumbi wa JNICC.