Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

ELIMU YA USALAMA YATOLEWA KILAMBO - MTWARA

Imewekwa: 11 February, 2026
ELIMU YA USALAMA YATOLEWA KILAMBO - MTWARA

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) leo tarehe 10 Februari, 2026 limeendelea kutoa Elimu ya Usalama wa Usafiri Majini kwa wakazi na wadau wa fukwe ya Kilambo mkoani Mtwara, ikiwa ni sehemu ya kuongeza uelewa na kuimarisha usalama wa shughuli za usafiri na usafirishaji majini.

Elimu hiyo imelenga kuwajengea uwezo wamiliki wa vyombo vya usafiri majini, waendesha vyombo, wavuvi, pamoja na wasafiri kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za usalama wakati wa usafiri na usafirishaji majini ili kuzuia ajali zinazoweza kuepukika.

Aidha, washiriki wameelimishwa kuhusu matumizi sahihi ya vifaa vya usalama ikiwemo jaketi okozi, umuhimu wa kufanya ukaguzi wa vyombo kabla ya safari, pamoja na kuzingatia taarifa za hali ya hewa kabla ya kuanza safari yoyote majini.

Maafisa wa TASAC wamewakumbusha wadau hao kuwa uzingatiaji wa sheria na kanuni za usafiri majini si hiyari bali ni wajibu wa kila mmoja, na kwamba kutokuzingatia masharti ya usalama kunaweza kusababisha madhara makubwa ikiwemo kupoteza maisha na mali.

Kwa upande wa wakazi na wadau wa fukwe ya Kilambo wameipongeza TASAC kwa kuendelea kuwafikia na kuwapatia elimu hiyo muhimu, wakieleza kuwa itaongeza usalama, kuimarisha shughuli zao za kiuchumi na kusaidia kulinda maisha ya watumiaji wa usafiri majini katika eneo hilo.

Elimu kuhusu Usalama, Ulinzi na Utunzaji wa Mazingira Majini mkoani Mtwara imeanza tarehe 9 Februari, 2026 na itaendelea hadi tarehe 13 Februari, 2026.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo