Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

Ushirikiano TASAC na wadau wa Usafiri kwa njia ya maji kuimarishwa.

Imewekwa: 19 January, 2024
Ushirikiano TASAC na wadau wa Usafiri kwa njia ya maji kuimarishwa.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala Meli Tanzania (TASAC), Bw. Mohamed Salum amepokea ugeni kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) siku ya Jumanne tarehe 9 Januari, 2024 katika ofisi za TASAC zilizopo jengo la PSSSF sakafu ya 8 jijini Dar Es salaam na kuzungumzia juu ya uboreshaji wa mawasiliano na ushirikiano kwa kuwa TASAC ni mtekelezaji wa  jukumu la udhibiti wa vyombo vya usafiri kwa njia ya maji na uchafuzi wa mazingira ya maji ambamo vyombo hivyo vinafanyia kazi.
Tanzania tuna eneo kubwa la ukanda wa bahari ya Hindi na maziwa makuu kama Ziwa Victoria, Tanganyika na Nyasa.
 
Ili kuratibu shughuli za uchukuzi majini zifanyike kwa  usalama tunahitaji mpango wa pamoja wa namna ya kuwasiliana kwa  wadau wote wa sekta ya uchukuzi majini. Aidha, TASAC  tuna jukumu la utafutaji na uokoaji pale ajali inapotokea au chombo cha usafiri majini kinapopata shida kwenye maji.
 
Bwana Mohamed Salum alisema, " Katika kutekeleza suala la utafutaji na uokoaji kila taasisi ina uwezo tofauti wa kutekeleza shughuli ya uokoaji. JWTZ, Polisi na Zimamoto mna vifaa na wataalam. Kwa hiyo kila mmoja wetu ana uwezo tofauti katika eneo analofanyia kazi. Hivyo kama taifa tunahitaji mpango wa pamoja wa mawasiliano yanayotuunganisha wote na yatambulike kisheria ili  kutekeleza jukumu hili".
 
"Kimataifa Shirika la Anga Duniani (International Civil Aviation Organization_ICAO) na Shirika la Bahari Duniani (International Maritime Organization-IMO) wana makubaliano ya pamoja ya Kidunia tangu mwaka 2002 ya namna ya kutafuta na kuokoa pale inapotokea ajali na Tanzania ni nchi mwanachama wa mashirika hayo. Hivyo hata ipo haja ya kuunganisha nguvu kama hayo mashirika" alisema Bwana.Mohamed Salum.
 
Pamoja na TASAC kuwa na Kamati ya Usalama na Ulinzi wa Usafiri Majini Kitaifa ambayo taasisi mbalimbli ni wajumbe na JWTZ wakiwemo bado suala la kuweka mikakati ya mawasiliano zaidi inahitajika ili kuepusha uchelewaji wowote wa kutoa huduma inayohitajika pale dharura inapotokea.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo