Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

UJUMBE WA TASAC WATEMBELEA MAMLAKA YA USAFIRISHAJI BAHARINI LIBERIA (LiMA)

Imewekwa: 02 October, 2025
UJUMBE WA TASAC WATEMBELEA MAMLAKA YA USAFIRISHAJI BAHARINI LIBERIA (LiMA)

Ujumbe kutoka Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), unaoshiriki Mkutano wa 8 wa Umoja wa Mamlaka za Usafirishaji Baharini Africa (AAMA), tarehe, 1 Oktoba, 2025 umetembelea makao makuu ya Mamlaka ya Usafirishaji Baharini Liberia (LiMA) uliopo jijini Monrovia.

Ujumbe huo umeongozwa na Wakili Leticia Mutaki kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, ulikaribishwa makao makuu ya LiMA na Kamishna Mkuu wa LiMA, Bw. Neto Zarzar Lighe ambaye ndiye Mtendaji Mkuu wa LiMA.

Ujumbe huo ulifanya mazungumzo na Bw. Lighe kujadili kuimarisha ushirikiano katika masuala ya usajili wa meli, usalama wa baharini, pamoja na kujengeana uwezo. 

Pande mbili pia zilibadilishana uzoefu kuhusu mfumo wa Rejesta ya Meli kwa Masharti Nafuu, ambapo Kamishna Lighe alitoa uzoefu wa Liberia, ambayo ni nchi inayoongoza kusajili meli nyingi duniani, na kushauri TASAC juu ya mwongozo muhimu kuhusu usajili wa meli na kuimarisha ushindani wa kimataifa katika sekta ya usafirishaji baharini.

Pia, walizungumzia uwezekano wa kusaini Hati ya Makubaliano (MoU) ili kuimarisha ushirikiano katika nyanja za usajili wa meli, mafunzo, ya mabaharia  pamoja na upatikanaji wa Sea time kwa mabaharia kutokana na u Liberia kuwa na meli nyingi kwenye regista yao jambo ambalo linawawezesha mabaharia wao kutokuwa na changamoto kabisa katika kupata Sea time.

Wakili Mutaki aliipongeza Liberia kwa uongozi wake katika sekta ya usafirishaji baharini na kusisitiza umuhimu wa mamlaka za usafirishaji baharini barani Afrika kushirikiana kwa karibu ili kukabiliana na changamoto zinazofanana, ikiwemo usafirishaji endelevu.

Wakati wa mkutano huo, Kamishna Mkuu Lighe aliomba TASAC kuunga mkono jitihada za  Liberia katika kuchaguliwa tena kuwa mjumbe wa Kundi A wa Baraza la Shirika la Kimataifa la Bahari Duniani (IMO) kwa kipindi cha 2026–2027. Liberia kwa sasa inashikilia kiti cha Kundi A, baada ya kuchaguliwa Desemba 2023 kwa kipindi cha 2024–2025. 

Kundi A linajumuisha nchi kumi zenye maslahi makubwa katika kutoa huduma za usafirishaji wa kimataifa, likijumuisha nchi kama Liberia, China, Marekani, Uingereza, na Japani.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo