TPA yaaswa kuboresha Bandari ya Bagamoyo
Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania -TASAC imeelekeza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kutatua changamoto zinazoikabili Bandari ya Bagamoyo.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Bodi hiyo Nah. Mussa Mandia wakati akizungumza na vyombo vya habari tarehe 24 Julai, 2024 mjini Bagamoyo. Bandari ya Bagamoyo ni bandari ya historia na imeendelea kutumika kwa mazingira hayo hayo ya asili ikiwemo kupwa na kujaa kwa maji.
"Tumeona bandari hii ina changamoto ya kupwaa kwa maji na kujaa, eneo ni la wazi, mahali pa kuwekea mizigo pako wazi na hakuna vifaa. Hali hii inazorotesha utendaji wa bandari. Ni jambo zuri TPA kutatua changamoto hizi hatua kwa hatua" Amesema Nah.Mussa Mandia.
Ameongeza kwa kusema "Tumeona kuna vifaa mbalimbali vimekusanywa hapa kwa ajili ya kuanza uboreshaji wa bandari ilahaitoshi. Ndio tunajua Serikali imetenga fedha za kujenga Bandari ya Mbegani, ila bado kuna umuhimu wa bandari ya kihistoria kuwepo ili kuhudumia vyombo vidogo. Kama mdhibiti ni vizuri tufahamu TPA ina mpango gani na bandari hii ambayo ni muhimu kwa vyombo vidogo na jamii."
Amesema Nah.Mussa Mandia.
Naye Afisa wa Forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Clara Medizedeck amesema kuna changamoto kubwa ya kudhibiti ukusanyaji wa mapato kwa sababu eneo la bandari halina uzio na lina uwazi mpana na mizigo inaweza kushushiwa mbali baharini na kuletwa kwa wapagazi.
Wakati huo Afisa msimamizi wa bandari hiyo Bw. David Kasembe amesema TPA imeanza kukusanya vifaa kwa ajili kufanya maboresho stahiki.
Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Mohamed Salum amesema, wanachukuwa maelekezo ya Bodi ya TASAC na watafutilia kwa karibu kuona bandari ya Bagamoyo inawekewa taa na paa kwa kuanzia ili kurahisisha kuhifadhi mizigo kwa usalama.
Bandari ya Bagamoyo inahudumia vyombo vingi vidogo ambavyo vinatoa huduma katika visiwa vya Unguja na Pemba kwa kupeleka vifaa vya ujenzi na vyakula. Aidha kuna vifaa pia vinaletwa Tanzania bara kupitia bandari hii.