TASAC, ZMA kuimarisha ushirikiano usimamizi wa Usafiri Majini
Ofisi ya Makamu wa Rais (SJMT) kwa kushirikiana na Wizara ya Uchukuzi (SMT), Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (SMZ), na Wizara ya Uchumi wa Buluu Zanzibar imeratibu kikao cha pamoja cha mashirikiano cha kujadili namna bora ya kuimarisha mashirikiano ya taasisi za usimamizi wa usafiri baharini.
Kikao hicho kimefanyika leo tarehe 02 Agosti 2024 kwenye Ofisi za Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar.
Kupitia kikao hicho taasisi za udhibiti wa usafiri majini, Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), chini ya Mkurugenzi Mkuu, Bw. Mohamed Salum na Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA), chini ya Mkurugenzi Mkuu, Bi Mtumwa Saidi ziliweza kujadili changamoto katika usimamizi wa usafiri majini nchini na kuzitafutia ufumbuzi. Kwa pamoja, TASAC na ZMA zimeafikiana maeneo watakayo shirikiana katika kusimamia masuala ya udhibiti na usimamizi wa usafiri baharini.
Kikao hicho, kilielekeza kuwa, ndani ya wiki mbili, kukamilishwa na kusainiwa kwa hati ya makubaliano ya utekelezaji wa mashirikiano katika masuala ya udhibiti wa usafiri baharini.
Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Mohamed Salum na Mkurugenzi Mkuu wa ZMA, Bi Mtumwa Saidi wameahidi kutekeleza maelekezo hayo kama yalivyotolewa kwenye kikao hicho.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (SMZ), Dkt. Mngereza Mzee Miraji, Katibu Mkuu Wizara ya Uchumi wa Buluu Zanzibar Hamad Bakar Hamad, Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais (SJMT) Abdallah Mitawi na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Dkt. Ally Possi.