Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

TASAC YAUNGANA NA WAFANYAKAZI NCHINI KUADHIMISHA MEI MOSI

Imewekwa: 04 May, 2026
TASAC YAUNGANA NA WAFANYAKAZI NCHINI KUADHIMISHA MEI MOSI

Wafanyakazi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) wameungana na wafanyakazi wenzao kutoka sekta mbalimbali nchini kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), wakisisitiza umuhimu wa kazi zenye staha katika kuchochea maendeleo ya taifa.

Maadhimisho ya kitaifa mwaka huu yamefanyika mkoani Njombe, ambapo Mgeni Rasmi alikua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Akizungumza katika Viwanja vya Lunyanywi, Rais Samia alisisitiza kuwa kazi zenye staha si tu chanzo cha kipato, bali ni msingi wa utu, heshima na maendeleo endelevu ya taifa.

Alieleza kuwa nguvu kazi yenye tija, inayofanya kazi katika mazingira bora na salama, ni nguzo muhimu katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa 2050. Aidha, alithibitisha dhamira ya Serikali kuendelea kuboresha ustawi wa wafanyakazi licha ya changamoto zilizopo, ili kuhakikisha wanakuwa na maisha bora na salama.

Mkoani Dar es Salaam, wafanyakazi wa TASAC walishiriki maadhimisho yaliyofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila. Katika hotuba yake, alimpongeza Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) kwa mchango wake katika kulinda maslahi ya wafanyakazi na kuimarisha mahusiano kati ya wafanyakazi na waajiri.

Alibainisha kuwa ushirikiano huo ni kichocheo muhimu cha kuongeza ufanisi katika taasisi na kuchangia maendeleo ya taifa kwa ujumla.

Kwa niaba ya wafanyakazi, Katibu wa Chama cha Walimu Mkoa wa Dar es Salaam, Mwl. Abraham Kamwela, aliwashukuru wafanyakazi kwa kujitokeza kwa wingi na kuwataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii huku wakizingatia sheria, kanuni na taratibu za kazi.

Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Mei Mosi mwaka huu ni: “Kazi zenye Staha ni Nguzo Imara kwa Maendeleo Endelevu katika Utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050.”

Mrejesho, Malalamiko au Wazo