TASAC YATOA ELIMU YA USAFIRISHAJI WA VILIPUZI NA MAKINIKIA GEITA

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Bw. Mohamed Salum amewatembelea na kutoa elimu kwa wadau mbalimbali wa Sekta ya Madini wanaoshiriki katika Maonesho ya Saba (7) ya Teknolojia ya Madini Geita, yanayofanyika katika Viwanja vya Bombambili Mkoani Geita.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Bw. Salum amesema lengo la TASAC kushiriki katika maonesho hayo ni kutoa elimu kwa wadau mbalimbali kuhusu majukumu ya Shirika ikiwemo usalama, ulinzi na utunzaji wa mazingira ya usafiri majini pamoja na masuala ya uondoshaji na ugomboaji wa shehena mahsus kama vile makinikia, vilipuzi pamoja na kemikali zinazotumika migodini.
“TASAC pamoja na shughuli za udhibiti wa usafiri majini pia tuna jukumu la kipekee la kusimamia masuala ya uondoshaji na ugomboaji wa madini kwa maana ya migodi mingi inasafirisha makinikia nje ya nchi kwa ajili ya uchenjuaji wa madini yaliyopo katika mchanga," amesema.
Ameongeza kuwa jukumu hilo linatekelezwa na TASAC hivyo wameshiriki maonesho hayo ili kutoa elimu wadau wa sekta ili waweze kutambua jukumu la Shirika katika kusafirisha bidhaa hizo.
Aidha ametoa wito kwa wadau kuzingatia masuala ya usalama waposafirisha mizigo kama vile vilipuzi na kemikali pamoja na vifaa vingine vinavyotumika katika ulipuaji.
“Migodi inatumia sana vilipuzi na inaagiza sana kemikali zote zinazotumika katika migodi ambapo TASAC ina wajibu wa kugomboa na kusafirisha hivyo tupo hapa kutoa uelewa kwa taasisi zilizokuwepo hapa kuwa kuna baadhi ya vifaa vinavyotumika katika ulipuaji visichanganywe na mizigo mingine wakati wa kusafirisha,” amesema Bw. Salum.
TASAC inashiriki katika maonesho hayo ambayo yalianza tarehe 02 Oktoba, 2024 na yanatarajiwa kufungwa kesho, Jumapili tarehe 13 Oktoba, 2024 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan.