Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

TASAC YATOA ELIMU KWA WANAWAKE IRINGA

Imewekwa: 04 March, 2025
TASAC YATOA ELIMU KWA WANAWAKE IRINGA

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limetoa elimu kwa wanawake na wasichana wa Mkoa wa Iringa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyoandaliwa na Shirika la Sauti ya Haki Tanzania, leo tarehe 3.3.2025 katika Ukumbi wa Mwananchi mjini Iringa.

Akitoa salamu za wadau mbalimbali Afisa Uhusiano Mwandamizi wa TASAC, Bi. Mariam Mwayela amewaasa wanawake na wasichana wa Iringa kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta ya usafiri majini.

“Nimesikia kuwa mna kikundi ambacho kinafanya miradi na tayari kuna mradi wa kulina asali basi sasa niwaase mje muwekeze katika sekta ya usafiri majini, kwani kuna fursa mbalimbali ikiwemo kufungua kampuni za usafi na upishi katika meli,” amesema Bi. Mwayela.

Aidha ameongeza kuwa jukumu la mwanamke katika jamii ni kuhamasisha watoto katika masuala ya elimu na hivyo mabinti wahamasishwe kuchangamkia fursa zilizopo nchini na nje ya nchi katika sekta ya usafiri majini.

“Kuna fursa nyingine ambazo mabinti zetu wanaweza kuchangamkia na kupata ajira kiurahisi ndani na nje ya nchi ikiwemo ubaharia, uhandisi na hata upishi katika meli ikizingatia kuwa watoto wetu wa kike tunawafundisha upishi tangu wakiwa wadogo hivyo ni rahisi kwao kusoma kozi hizo na kupata ajira” ameongeza Bi. Mwayela.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa TAMCODE, Bi. Rose Kunangwa amesema kuwa taifa, halina budi kujipongeza kwa hatua kubwa iliyopiga katika kumtambua na kumuwezesha mwanamke katika sekta za kiuchumi, kisiasa, kijamii, na kiutamaduni.

“Siku kama ya leo ni siku ya kutafakari ni mikakati gani inafaa tuiweke kuboresha na kuwezesha fursa sawa kwa wote katika sekta ya siasa, uchumi na utamaduni ili tuweze kumuinua mwanamke na msichana kutoka hapa tulipo na kusonga mbele zaidi.

Wakili Leticia Petro ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Sauti ya Haki ambao ni waratibu wa maadhimisho hayo ameishukuru TASAC kwa kuwezesha maadhimisho hayo pamoja na kutoa elimu kuhusu usafiri majini na fursa zinazopatikana katika sekta hiyo.

Kaulimbiu ya Siku ya wanawake Duniani mwaka huu ni Wanawake na Wasichana 2025: Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo