Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

TASAC YATOA ELIMU KISIWA CHA BWIRO-UKEREWE

Imewekwa: 16 October, 2025
TASAC YATOA ELIMU KISIWA CHA BWIRO-UKEREWE

Katika kuendelea kutoa elimu ya usalama katika usafiri majini nchini, Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) jana tarehe 15 Oktoba,  2025 limetoa elimu kwa wadau mbalimbali katika kisiwa cha Bwiro wilayani Ukerewe mkoani Mwanza.

Akizungumza na wadau wakati wa utoaji elimu kwa wadau mbalimbali wa usafiri majini katika Kisiwa hicho Afisa Mfawidhi wa TASAC Wilaya ya Ukerewe Naho. Michael Rogers amesema moja ya majukumu ya TASAC ni kusimamia masuala ya Ulinzi, Usalama na Utunzaji wa Mazingira ya Usafiri Majini na kuhakikisha wadau wanaotumia vyombo hivyo, mizigo pamoja na vyombo vinakuwa salama.

“TASAC ina utaratibu wa kusimamia vyombo vinavyosafirisha abiria na mizigo kwenye maji na tunashirikiana na vyombo mbalimbali kupata taarifa pindi kunapokuwa na ukiukwaji wa sheria na hatua za kisheria huchukuliwa kwa wadau hao ikiwa ni pamoja na kuwatoza faini ama kufungia vyombo. 

Naho. Rogers ameongeza kuwa ni jukumu la wamiliki na waendeshaji wa vyombo kuhakikisha wanazingatia usajili wa chombo na shughuli wanazozifanya na si vinginevyo.

“Chombo kilichosajiliwa kubeba mizigo hakitakiwi kubeba abiria na pia vyombo kwa ajili ya kusafirisha abiria viwe na vifaa vya uokoaji ikiwemo jaketi okozi za kutosha abiria wote  ikiwa ni pamoja na ziada ya asilimia 10 kwa watoto,” amesema Naho. Rogers.

Nao wakazi wa kisiwa hicho wameiomba Serikali kuona uwezekano wa kupunguza gharama za ununuzi wa maboya na kurahisisha upatikanaji wa vifaa hivyo kwenye maeneo yao ili kuimarisha zaidi usalama wao pindi wanapokuwa kwenye safari za majini kwa kuwa baadhi ya wamiliki wa vyombo wanashindwa kuwa na idadi kamili ya maboya kwenye vyombo vyao kutokana na changamoto ya gharama na uhaba wa vifaa hivyo kwenye maeneo yao.

TASAC inaendelea na utoaji wa elimu kwa wadau mbalimbali ili kuhakikisha elimu ya usalama katika usafiri majini inawafikia wadau wengi ili kufikia lengo la kutokuwa na ajali na vifo katika usafiri majini.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo