Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

TASAC YASHIRIKI MAPOKEZI YA MWILI WA BAHARIA ALIYEFARIKI KATIKA MFEREJI WA HORMUZ

Imewekwa: 19 May, 2026
TASAC YASHIRIKI MAPOKEZI YA MWILI WA BAHARIA ALIYEFARIKI KATIKA MFEREJI WA HORMUZ

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), leo Mei 18, 2026, limeshiriki mapokezi ya mwili wa baharia Mtanzania, Nahodha Mchama Maregesi Mongu, uliowasili jijini Dar es Salaam kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere.

Akizungumza wakati wa mapokezi ya mwili huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TASAC, Nahodha Mussa Mandia, ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwezesha mchakato mzima wa kurejesha mwili wa marehemu nchini.

“Tunatoa shukrani za dhati kwa Serikali kwa kuhakikisha mwili wa Nahodha mwenzetu, Mchama Mongu, unarejeshwa nyumbani salama. Kwa namna ya kipekee tunaishukuru Wizara ya Mambo ya Nje kwa jitihada kubwa zilizofanyika hadi kufanikisha hatua hii muhimu,” alisema Nahodha Mandia.

Aidha, Nahodha Mandia ameziasa kampuni zinazomiliki na kuendesha meli kuendelea kuzingatia sheria, kanuni na viwango vya kimataifa vya usalama na ulinzi wa mabaharia ili kupunguza hatari zinazoweza kuwakumba wafanyakazi wanapokuwa kazini.

Kwa upande wa ndugu wa marehemu wameishukuru Serikali pamoja na TASAC kwa ushirikiano na juhudi zilizowezesha mwili wa ndugu yao kurejeshwa nchini kwa ajili ya mazishi.

Nahodha Mongu alifariki dunia tarehe 3 Mei 2026 katika Mfereji wa Hormuz nchini Iran akiwa kazini ndani ya meli ya kuvuta (tug boat) iitwayo VOLANS, inayopeperusha bendera ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), iliyokuwa ikisafiri kutoka UAE kuelekea Oman.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo