TASAC YASHIRIKI MAFUNZO YA ULINZI WA MELI ZA KIMATAIFA NA MIUNDOMBINU YA BANDARI (INTERNATIONAL SHIP AND PORT FACILITY SECURITY (ISPS ) CODE
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limeshiriki Mafunzo ya Ulinzi wa Meli za Kimataifa na Miundombinu ya Bandari (ISPS Code) kwa Maafisa Ulinzi wa Miundombinu ya Bandari (Port Faficility Security Officers - PFSO).
Mafunzo hayo yenye lengo la kuwajengea uwezo katika masuala ya ulinzi wa miundombinu ya bandari na Meli za Kimataifa ziwapo katika bandari nchini yanafanyika katika Hoteli ya Protea, jijiniDar es Salaam.
Akizungumza katika mafunzo hayo wakati wa ufunguzi leo tarehe 30 Septemba, 2024, Mgeni Rasmi katika hafla hiyo Bw. Lucas Kambelenje, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Wizara ya Uchukuzi amewataka maafisa ulinzi waliopata fursa ya kushiriki mafunzo hayo kuyatumia vizuri ili kuleta chachu katika utekelezaji wa ISPS Code.
Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Udhibiti Usafiri Majini TASAC, Bw. Julius Mitinje kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TASAC amewashukuru wakufunzi kwa kutoa mafunzo hayo kwa Watanzania.
"Nawasihi mushiriki ipasavyo ili mafunzo haya yawe yenye manufaa katika Sekta ya Usafiri Majini," amesema.
Wadau mbalimbali wameshiriki ufunguzi wa mafunzo hayo ambao ni pamoja na Wizara ya Uchukuzi, TASAC, Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Usafiri Majini Zanzibar (ZMA), Mamlaka ya Bandari Zanzibar (ZPC), na DP World.
Mafunzo hayo yanafanyika kwa siku tano yanayotolewa na Shirika la Bahari Duniani (IMO) kuanzia leo tarehe 30 Septemba hadi tarehe 4 Oktoba, 2024.