TASAC YASHIRIKI MAADHIMISHO SIKU YA WANAWAKE DUNIANI

Watumishi wanawake wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), leo tarehe 8 Machi, 2025 wameungana na wanawake wote nchini Tanzania katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, iliyofanyika kitaifa jijini Arusha.
Maadhimisho hayo yamefanyika kwa kufanya maandamano yaliyopokelewa na Mgeni Rasmi wa Maadhimisho hayo, Mheshimiwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika viwanja vya Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Katika hotuba yake Mheshimiwa Rais ameeleza jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita katika kushirikisha wanawake wachapakazi katika uongozi ili kufikia malengo ya kitaifa.
"Ni dhahiri kuwa tumeweza kujionea wanawake mbalimbali wakipita hapa katika maandamano wakionesha kazi wanazozifanya kwa umahiri mkubwa wakiwakilisha sekta mbalimbali hapa nchini," amesema.
Wakati huo huo, watumishi wanawake wa TASAC Makao Makuu walikua ni miongoni mwa wanawake waliohudhuria maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani mkoa wa Dar es Salaam yaliyofanyika katika viwanja vya Leaders' Club ambapo Mgeni Rasmi alikua Mhe. Albert Chalamila Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Kauli Mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake mwaka huu ni: “Wanawake na Wasichana 2025: Tudumishe Haki. Usawa na Uwezeshaji.”