TASAC YASHIRIKI KIKAO CHA WADAU KUHUSU KITUO CHA NJOC KUIMARISHA ULINZI WA BAHARINI

Shirika la Uwakala Meli Tanzania (TASAC), tarehe 13 Juni, 2025 lilishiriki kikao cha viongozi na wadau wa taasisi mbalimbali za Serikali kutoka Tanzania Bara, Visiwani na wadau wa Kimataifa ili kujengeana uelewa kuhusu Kituo cha Kitaifa cha Uratibu wa pamoja wa Ulinzi na Usalama Baharini (National Joint Operations Centre - NJOC), kilichofanyika Ukumbi wa Mikutano wa Jengo la Mnara wa Kuongozea Meli (Ship Traffic Tower), jijini Dar es Salaam.
Kikao hicho kilifunguliwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Dkt. Habiba Omar, ambaye alisema uanzishwaji wa NJOC ni hatua muhimu ya kuhakikisha usalama na ulinzi wa baharini hasa kwa kuzingatia ongezeko la vitisho vya kimataifa hivyo ni muhimu kuja na mikakati pamoja ya kujilinda.
Naye Mkurugenzi wa Usalama na Mazingira kutoka Wizara ya Uchukuzi, Bi. Stella Katondo alitoa shukrani kwa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC) na Idara ya Nchi za Nje ya Marekani (INL) kwa kusaidia ukarabati wa kituo na kutoa mafunzo kwa watumishi wake hatua ambayo imeimarisha uwezo wake wa kitaalamu na kiutendaji.