TASAC YASHIRIKI DORIA YA ULINZI NA USALAMA BAHARINI
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa kushirikiana na Jeshi la Wanamaji Tanzania (Navy) kupitia Kituo cha “National Joint Operation Center (NJOC)”, wamefanya doria ya ulinzi na usalama baharini hususan katika eneo la meli zinazosubiri kuingia bandarini (outer anchorage) ili kudhibiti vitendo vya kihalifu vinavyoweza kutokea baharini.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, lililofanyika katika Pwani ya Bahari ya Hindi, jijini Dar es Salaam, jana tarehe 07 Januari, 2025, Nah. Ghadafi Chambo wa TASAC amesema kuwa doria hiyo imefanyika ili kuzuia uwepo wa vitendo vya kihalifu baharini kwa vyombo vya usafiri majini vinavyotoka katika bandari bubu kufanya biashara ya kuuza bidhaa pasipo kufuata taratibu za kiforodha.
"Kumekuwepo tabia ya baadhi ya watu kufanya biashara na meli zilizopo nangani katika eneo la maji ya bandari (outer anchorage)," amesema Nah. Chambo.
Nah. Chambo ameeleza kuwa ili kudhibiti hali hiyo pamoja na uhalifu mwingine baharini, TASAC imeamua kushirikiana na vyombo vya ulinzi hususan Jeshi la Wanamaji ili kudhibiti uhalifu wa namna hiyo ikiwa ni pamoja na kulinda mazingira ya bahari yanayoweza kuchafuliwa na shughuli zinazofanyika melini hususani umwagaji holela wa mafuta yanayoendeshea mitambo ya meli.
Aidha, Boti hiyo ya Doria ambayo ilikabidhiwa kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 21 April, 2024 kupitia kwa ufadhili wa Serikali ya Japan kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Tanzania chini ya Mradi wa Kukabiliana na Vitendo vya Kihalifu katika Bahari na Maziwa Makuu nchini na inaendelea kutekeleza majukumu yake katika ukanda wa pwani ya Tanzania.
Boti hiyo ambayo ni ya kisasa na yenye uwezo mkubwa wa kufanya doria kwa muda mrefu, imeongeza ufanisi katika suala la Ulinzi katika maji ya Tanzania ikiwa ni pamoja na Kuimarika kwa Usalama wa “Single Point Mooring (SPM) na Visiwa vidogo vinavopatikana nje kidogo ya mlango wa kuingilia katika Bandari ya Dar es Salaam.