TASAC YARIDHIKA NA UTOAJI HUDUMA ZA BANDARI BAADA YA MAELEKEZO YA MHESHIMIWA RAIS
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limeeleza kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa agizo la kuendelea na shughuli za kiuchumi mara baada ya Uchaguzi Mkuu, lililotolewa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan mnamo tarehe 3 Novemba, 2025.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, leo, tarehe 7 Novemba 2025, wakati wa ziara ya ukaguzi katika Bandari ya Dar es Salaam, Meneja wa Uhusiano na Masoko wa TASAC, Bw. Saidi Mkabakuli, amesema kuwa TASAC imejiridhisha kuwa shughuli zote za upakuaji na upakiaji shehena zinaendelea kwa vizuri na kwa ufanisi mkubwa kama ilivyokua awali.
“Tunaendelea kutekeleza maagizo ya Mheshimiwa Rais kwa vitendo. Huduma zote bandarini sasa zinatolewa bila mkwamo wowote na naomba niwahakikishie wadau wote kuwa huduma zinatolewa vizuri na kwa ufanisi mkubwa kama ilivyokua awali,” amesema Bw. Mkabakuli.
Aidha, Bw. Mkabakuli ametoa wito kwa wadau wa sekta ya usafirishaji na biashara kuendelea kutumia bandari za Tanzania kwa kuwa mazingira ya utoaji huduma yameboreshwa zaidi, huku TASAC ikiendelea kushirikiana kwa karibu na mamlaka nyingine katika kukuza ufanisi wa sekta ya uchukuzi kwa njia ya maji.
“TASAC inasimamia utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ili kuhakikisha wadau hawakwami katika biashara zao ukizingatia Tanzania ni lango kuu na kitovu cha upitishaji shehena kwa upande wa nchi za Afrika Mashariki,” ameongeza.
Kwa upande wake Meneja Uhusiano wa Kampuni ya DP World Tanzania, Bw. Elitunu Mallamia kuwa kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za Serikali wameendelea kutekeleza maelekezo ya kuhudumia ushushaji na upakiaji wa shehena kwa ufanisi zaidi hasa mara baada ya kurejea kwa huduma ya mtandao.
Ameeleza kuwa taasisi zote zinazohusiana na huduma za bandari zimeimarisha miundombinu, mifumo ya usalama, na utendaji wa huduma, hatua inayolenga kuhakikisha wateja wanapata huduma bora na za uhakika bila ucheleweshaji.