TASAC- YARIDHIKA NA MABORESHO YA BANDARI YA BUKOBA NA KEMONDO

Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania -TASAC imeridhika na maboresho ya ujenzi wa bandari ya Bukoba na Kemondo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 24 Aprili, 2025 katika bandari ya Bukoba mkoani Kagera, Mwenyekiti wa Bodi Nah. Mussa Mandia, amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita imewekeza shilingi bilioni 19.5 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya bandari ya Bukoba ambao kwa sasa umefikia asilimia 98. Kwa uoande wa bandari ya Kemondo, jumla ya shilingi bilioni 20 zimetumika mbapo mradi umekamilika kwa asilimia 100 na kukabidhiwa Novemba 30, 2024. Ujenzi huo utawezesha meli pamoja na boti kutumia bandari hizo kwa kusafirisha mizigo na abiria wanaokwenda sehemu mbalimbali zikiwemo visiwa vilivyopo katika Ziwa Victoria pamoja na nchi jirani kama vile Kenya na Uganda. Pia itafungua fursa za uchumi kwa wananchi wa Mkoa wa Kagera na mikoa jirani.
"Tunampongeza Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuruhusu kutumia fedha hizo kujenga bandari hizi mbili. Bandari hizi zitahudumia meli kubwa ya Mv. Mwanza na New Mv. Victoria, Hapa Kazi Tu, pamoja na meli nyingine. "Tunawaomba Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) pamoja na wananchi kuzitunza na kuzitumia bandari hizi katika kutoa huduma ya usafiri majini."
Ameongeza kuwa "wananchi wawe tayari kufuata maelekezo, sheria na kanuni zilizowekwa na bandari ili huduma ya usafiri majini iwe salama na endelevu ", amesema Nah. Mandia.
Naye Bw. David Nicodem, Kaimu Mkuu wa Bandari ya Kemondo, ameishukuru Bodi hiyo na kuahidi kuzingatia ushauri walioutoa.
"Hakika kwa sasa bandari imekamilika kwa asilimia 100, na sasa tuna magati matatu ya kuhudumia meli kubwa na gati lingine la kuhudumia vyombo vidogo.
Aidha, wafanyabiashara wamerudi kwa wingi wanatumia bandari hii. Shehena imeongezeka kutoka tani 300 tulizokuwa tunahudumia hapo awali hadi kufikia tani 400 kwa mwezi na mapato yamepanda kutoka shilingi milioni 23 hadi milioni 75 kwa mwezi", amesema Bw. Nicodem.
Kwa upande wake, Afisa Bandari ya Bukoba, Bw. Malick Ismaili amesema kuwa ujenzi wa bandari unaoendelea ukikamilika, bandari hiyo itatoa huduma nzuri zaidi kuliko hapo awali kwa sababu bandari itakuwa na uwezo wakuhudumia meli 4 kwa wakati mmoja kuliko sasa ambapo ina uwezo wa kuhudumia meli moja tu kwa ufanisi. Pia, vyombo vidogo vimejengewa gati mbili kwa ajili ya kuhudumia visiwa vilivyopo katika ziwa Victoria.
" Ujenzi wa Bandari ya Bukoba wenye thamani ya shilingi bilioni 19.5 umefikia asilimia 98 sasa na unatarajia kukamilika mwishoni mwa mwezi Aprili, 2025. Majengo ya abiria na mifumo ya usalama imejengwa na kuwekwa vizuri."
Aidha, Bodi hiyo imeshauri Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania kuweka watumishi weledi katika kusimamia huduma za bandari hiyo ili iweze kuleta tija stahiki.
Ziara ya Bodi ya Wakurugenzi TASAC inafanya ukaguzi wa shughuli za TASAC na kukutana na wadau mbalimbali wa sekta ya usafiri majini katika mialo ya ziwa Victoria iliyopo wilaya ya Muleba na katika maziwa madogo yaliyopo wilayani Karagwe.