TASAC YARATIBU KIKAO CHA KUKUSANYA MAONI YA WADAU KUHUSU KURIDHIA KIAMBATISHO CHA SITA CHA MKATABA WA KIMATAIFA WA KUZUIA UCHAFUZI WA MAZINGIRA YA BAHARI

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) chini ya Wizara ya Uchukuzi, leo tarehe 10 Machi, 2025 limeratibu kikao cha wadau wa sekta ya uchukuzi majini ili kupokea maoni ya juu ya Tanzania kuridhia Kiambatisho cha Sita cha Mkataba wa Kimataifa wa Kuzuia Uchafuzi wa Mazingira Unaotokana na Shughuli za Meli Baharini wa Mwaka 1973/1978, au kwa kifupi MARPOL ANNEX VI.
Akizungumza wakati wa kufungua kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Utalii kilichopo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Sera na Mipango wa Wizara ya Uchukuzi, Bw. Maseke Mabiki, kwa niaba ya Katibu Mkuu amesema kuwa udhibiti wa uchafuzi mazingira ni suala nyeti duniani kote na kuridhia kwa kiambatisho hicho kutatoa fursa kwa nchi kudhibiti uchafuzi wa hewa unaotokana na uchomaji wa gesi za ukaa katika meli na kuiwezesha nchi kukagua meli za ndani na kimataifa kuhusu uchomaji wa gesi za ukaa zinazopelekea kuathiri Tabaka la Ozoni.
Ameongeza kuwa Tanzania mpaka sasa imeridhia viambatisho vitano vya Mkataba huo ambavyo vinahusu udhibiti wa uchafu unaotoka na mafuta, vimiminika hatarishi vinavyotoka kwenye meli, na kuzuia vitu hatarishi kutokana na vifungashio kwenye meli, pamoja na kuzuia uchafuzi unaotokana na maji taka na taka ngumu melini.
“Naomba nitoe wito kwenu, kupitia kwa umakini andiko hili ili kuangalia manufaa ya kimazingira, kiuchumi na kijamii yatakayopatikana kutokana na kuridhia kwa kiambatisho hicho,” amesema Bw. Mabiki.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Sheria TASAC, Wakili Judith Kakongwe kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TASAC amesema wadau ni jicho la pili linalosaidia kupanua wigo wa mawazo ya wataalam katika kuboresha maandiko ya kitaalam.
"Ni vema tufahamu taifa lina nia njema kuridhia itifaki hii itakayodhibiti uchafuzi wa hewa zinazotokana na shughuli za meli hivyo ni muhimu tujielekeze huko dunia inakoenda na kutazama namna ya kunufaisha taifa na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi," amesema Wakili Kakongwe.
Kikao kingine cha kukusanya maoni kitafanyika tarehe 12 Machi, 2025 Visiwani Zanzibar. Wadau wameombwa kuendelea kutoa maoni kwa njia ya maandishi ili kuweza kuboresha andiko hilo.