TASAC YAPONGEZWA UJENZI WA KITUO CHA UTAFUTAJI NA UOKOZI

Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa amelipongeza Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa kutekeleza ujenzi wa Kituo cha Utafutaji na Uokoaji katika Ziwa Victoria (MRCC) kilichopo katika eneo la Ilemela, jijini Mwanza na ujenzi vituo vingine vidogo vitatu (3) katika maeneo ya Kanyala, Ukrerewe na Mara.
Prof. Mbarawa ametoa pongezi hizo wakati alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hiko, leo tarehe 24 Januari, 2025.
Kadhalika, Prof. Mbarawa ameipongeza TASAC kwa kusimika minara na vifaa vya mawasiliano katika Ziwa Victoria ambavyo vitasaidia pindi ajali za majini zitakapotokea.
Prof. Mbarawa ameiagiza TASAC kuendelea kununua vifaa vya kisasa vya uokoaji ikiwemo boti ziendazo kasi ili zisaidie kufika kwenye matukio kwa haraka ili kuwawezesha wananchi wanaofanya shughuli za kiuchumi majini kuwa usalama zaidi ili pindi ajali za majini zinapotokea.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Hamid Mbegu, amesema tayari shirika hilo limeanza kutekeleza agizo hilo kwa vitendo na kubainisha kuwa katika mwaka huu wa fedha TASAC imepanga kununua boti mbili za uokoaji.
"Pamoja na boti hizi mbili, kwa mwaka ujao wa fedha tumepanga kununua boti tatu za uokoaji ambapo jumla tutakuwa na boti tano. Tumezingatia viwango vya kisasa," Bw. Mbegu ameeleza.
Mratibu wa mradi huo, Nahodha Emmanuel Marijani, amesema ujenzi wa kituo hicho umefikia asilimia 70.