TASAC YAPONGEZWA KUTOA ELIMU YA USALAMA KWA WASAFIRI MAJINI
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), leo, tarehe 9 Februari, 2026, limepongezwa na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara, Bw. John Tilubuzya, kwa kuendelea kutoa elimu kwa wadau mbalimbali wanaotumia usafiri majini.
Bw. Tilubuzya ametoa pongezi hizo alipokutana na kufanya mazungumzo na maafisa wa TASAC walipotembelea ofisini kwake kwa lengo la kujitambulisha na kupata ridhaa ya kutoa elimu kwa wadau mbalimbali katika mialo iliyopo Mkoa wa Mtwara.
“Nawakaribisha kwa dhati katika Mkoa wa Mtwara na nawapongeza sana kwa juhudi zenu za kuendelea kuelimisha umma kuhusu usafiri majini. Kazi mnayoifanya ni muhimu sana katika kuhakikisha usalama wa vyombo vya usafiri majini pamoja na kuwalinda watumiaji wake, na ina mchango mkubwa katika kuimarisha usalama na uelewa kwa wananchi,” amesema Bw. Tilubuzya.
Aidha, Bw. Tilubuzya ameahidi kuwepo kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa na TASAC katika kufanikisha majukumu ya kuhakikisha usalama wa vyombo vya usafiri majini na watumiaji wake. Amesema ofisi yake iko tayari kushirikiana na TASAC katika shughuli mbalimbali za uelimishaji kwa umma na usimamizi ili kuongeza uelewa wa masuala ya usalama kwa wadau wote.
Elimu kuhusu Usalama, Ulinzi na Utunzaji wa Mazingira Majini mkoani Mtwara imeanza leo tarehe 9 na itaendelea hadi tarehe 13 Februari, 2026.