Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

TASAC YAPONGEZA WATOA HUDUMA USAFIRI MAJINI KUZINGATIA SHERIA NA KANÙNI

Imewekwa: 19 December, 2024
TASAC YAPONGEZA WATOA HUDUMA USAFIRI MAJINI KUZINGATIA SHERIA NA KANÙNI

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limepongeza watoa huduma ya usafiri majini kwa kubeba abiria kwa mujibu wa matakwa ya masharti ya leseni walizopewa ili kusafirisha abiria kwa usalama.

Hayo yamesemwa na Mkaguzi Mwandamizi wa TASAC, Mhandisi Rashid Katonga, leo tarehe 18 Desemba,2024, jijini Dar es Salaam, wakati akiendelea na zoezi la ukaguzi wa boti zinazotoa huduma ya usafiri kati ya Dar es Salaam na Zanzibar.

Mhandisi Katonga amesema kuwa TASAC imeongeza nguvu za kufanya ukaguzi wa vyombo vya usafiri majini ili kuhakikisha usalama wa abiria unaimarishwa hasa katika kipindi hiki cha uhitaji wa huduma ya usafiri majini. 

"Ni utaratibu wa TASAC kufanya  ukaguzi kila  inapofika mwisho na mwanzo wa mwaka kwa sababu abiria huwa ni wengi wanaotaka kusafiri kuliko vyombo vya usafiri vinavyotoa huduma hiyo. Kutokana hilo tunataka wasafiri na wasafirishaji waendelee kufuata kanuni na taratibu za usalama ili wasafiri kwa usalama," amesema Mhandisi Katonga.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Kampuni ya Zanzibar Fast Ferries, Naho. Donald Mfundo, ameipongeza TASAC kwa kufanya kaguzi hizo hasa katika kipindi cha mwisho wa mwaka ambapo kumekua na ongezo la abiria.

Naho. Mfundo amezungumzia tabia ya abiria wanaopenda kukaa kwenye viti vya nje ya boti maeneo ya mbele na nyuma kuwa ni sehemu mojawapo ya ya kupata hewa safi na kuwa ni sehemu ya kufanya utalii wa bahari.

“Kuna tabia ya abiria wanaopenda kukaa kwenye maeneo ya viti vya nje ya boti mbele na nyuma, sisi kama waendeshaji wa vyombo hivi tunakua makini sana kwa kuwaweka chini ya uangalizi wa mabaharia wakati wote wa safari, ili pale inapotokea tatizo waweze kupata msaada wa haraka,” amesema Naho. Mfundo.

TASAC imendelea na zoezi la ukaguzi wa vyombo vya usafiri majini ambalo ni endelevu na hufanywa kwa nchi nzima ili kuhakikisha wamiliki na waendesha wa vyombo vya usafiri majini wanazingatia matakwa ya leseni zao.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo