TASAC yapokea kilio cha wavuvi Mafia
Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) ikiongozwa na wenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TASAC, Nah. Mussa Mandia imefanya ziara ya kukutana na wavuvi, waendeshaji wa vyombo vidogo vya uvuvi Wilaya ya Mafia mkoani Pwani siku ya Jumatatu tarehe 22 Julai, 2024 na kusikiliza kilio cha kuhitaji kuimarisha usalama wa vyombo vidogo vya usafiri majini.
Akizungumza katika mkutano huo Nah. Mussa Mandia amesema kuwa moja ya majukumu ya TASAC ni kufanya ukaguzi na kusimamia usalama wa vyombo vya usafiri majini.
"Nafahamu maisha ya wavuvi ni baharini ambapo ndipo wanapata kipato cha kuendesha maisha na wengi wenu ni nadra kutumia maboya. Ili muwe salama TASAC inabidi kuhakikisha vyombo vina maboya na tunakuwa tayari kuokoa kwa haraka pale inapotokea ajali. Mkurugenzi Mkuu yupo hapa amepokea ombi lenu la kuona namna ya kuwa na chombo cha uokozi na kuendelea kutoa elimu ya usafiri salama majini." Amesema Nah. Mussa Mandia.
Nao wavuvi wa Mafia kupitia katibu wa Umoja wa Wavuvi, Bw. Mohamed Tego wameiomba TASAC kuimarisha usalama wa usafiri majini kwa kuwapatia vyombo vya uokozi ili kusaidia kuokoa watu pale ajali za majini zinapotokea.
"Sisi wavuvi usiku na mchana tupo majini kutafuta riziki na huwa inatokea watu wanapata ajali na tunachanga na kuwatafuta hata hivyo wakati mwingine wanapatikana na wengine wanapotea jumla na chombo. Lakini chombo kikiwepo ni rahisi kukitumia kwa kwenda kwa uharaka kwenye tukio." Amesema Bw. Tego.
Aidha, Bw. Tego ameongeza kuwa Kisiwa cha Mafia kina samaki wakubwa duniani ambao ni kivutio cha utalii, ameiomba TASAC kuelekeza Meli zinapofika ukanda wa bahari eneo la Mafia zipunguze mwendo na kujiepusha na kuchafua mazingira ya samaki na mazalia yao ambao ndio uti wa mgongo wa uchumi wa Mafia.
Ziara hii ya wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi TASAC imeanza tarehe 22 Julai, 2024 katika Wilaya ya Mafia, itafutia Nyamisati, Bagamoyo na kuhitimishwa tarehe 27 Julai, 2024 katika mwalo wa Mkwaja Mkoani Tanga.