TASAC YAPEWA KONGOLE NA TRA
Meneja wa Mamlaka ya Mapato (TRA) Mkoa Kodi wa Ilala, Bi Eva Raphael amelipongeza na kulishukuru Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) kwa ulipaji wa kodi kwa usahihi na kwa wakati hali inayoongeza pato la Taifa.
Ameyasema hayo, leo, tarehe 17 Desemba,2024 katika ofisi za TASAC zilizopo jengo la SUMATRA, jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya kuwatembelea wadau wa Mkoa wa Kodi wa Ilala na kuwapongeza kwa kulipa kodi kwa usahihi na wakati.
"Sisi TRA tunajisikia vizuri kwa kushirikiana na TASAC katika kulipa kodi kwa usahihi na wakati bila usumbufu, utamaduni huu ni mzuri na unasaidia kutumia kodi kwa ajili ya kuwahudumia wananchi," amesema.
Ameongeza kuwa kwa kutambua mchango wa TASAC katika kulipa kodi kwa wakati, TRA imelizawadia Shirika na kutoa wito wa kuendelea na utamaduni huo mzuri wa kulipa kodi sahihi na kwa wakati.
Zawadi hizo zimepokelewa na Mkurugenzi wa Fedha na Uhasibu wa TASAC, CPA Pascal Kalomba kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TASAC.
CPA Kalomba amesema kuwa TASAC itaendelea kutoa ushirikiano wa karibu kwa TRA ili Serikali ipate mapato stahiki yatakayosaidia kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini.
"Sisi kama taasisi ya Umma tutaendelea kutoa ushirikiano kwa TRA kwa kulipa kodi stahiki na kwa wakati," ameahidi CPA Kalomba.
Tangu kuundwa kwa TASAC, imekua ikifanya kazi kwa karibu na TRA hali ambayo imewezesha kuongeza tija katika ulipaji wa kodi stahiki na kwa wakati hali inayokuza mapato ya Serikali.