Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

TASAC YAKUTANISHA WADAU KUJADILI TARATIBU ZA USAFIRISHAJI WA BIDHAA NJE YA NCHI

Imewekwa: 07 August, 2025
TASAC YAKUTANISHA WADAU KUJADILI TARATIBU ZA USAFIRISHAJI WA BIDHAA NJE YA NCHI

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), leo tarehe 6 Agosti 2025 limekutana na wadau wa sekta ya uchukuzi wanaoendesha shughuli za forodha kwa lengo la kuhamasisha kuhusu taratibu za usafirishaji nje wa bidhaa na kubainisha changamoto za kiutendaji.

Akifungua kikao hicho, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Nahson Sigalla ambaye ni Mkurugenzi wa Udhibiti Uchumi TASAC amesema kuwa lengo kuu la TASAC kama mdhibiti ni kuchochea ufanisi katika utoaji huduma ili kuboresha mnyororo mzima wa huduma za uondoshaji shehena.

“TASAC kama mdhibiti tunahimiza ufanisi katika utoaji wa huduma ili kuongeza ushindani katika huduma za usafiri majini  hivyo tunawataka wadau watoe maoni yao kwa lengo la kuboresha mnyororo mzima wa uondoshaji shehena,” amesema Bw. Sigalla.

Ameongeza kuwa TASAC inaendelea kupitia na kupendekeza maboresho ya kuhuisha sheria na kanuni mbalimbali zinazosimamiwa na Shirika ili kuhakikisha kuwa sekta ya usafiri majini inakuwa bora na yenye ufanisi.

Kwa upande wake, Bw. Ramadhan Masano kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) amesema kuwa lengo la mfumo ulioboreshwa wa TANeSWs ni kurahisisha uondoshaji wa mizigo katika bandari, viwanja vya ndege, na maeneo ya mipakani.

“Uboreshaji wa mfumo ni mchakato endelevu kwa kuboresha na kuhuisha mfumo  ili kuongeza ufanisi, utendaji kazi, na urahisi wa matumizi kwa watumiaji. Maboresho haya ni muhimu sana ili kuendana na mahitaji yanayobadilika ya biashara ya kimataifa, maendeleo ya kiteknolojia, pamoja na matakwa ya kisheria na kikanuni,” amesema Bw. Masano.

Kikao hicho kilikutanisha wadau kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Chama cha Waendeshaji Bandari Kavu (CIDAT), Vyama vya Mawakala wa Forodha (TAFFA, TACAS na CALAT).

Mrejesho, Malalamiko au Wazo