Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania

ISO 9001:2015 Certified

TASAC YAKUTANA NA WASAFIRISHAJI NA MAWAKALA WA FORODHA KUJADILI USAFIRISHAJI WA SHEHENA ZA MAKONTENA

Imewekwa: 15 May, 2026
TASAC YAKUTANA NA WASAFIRISHAJI NA MAWAKALA WA FORODHA KUJADILI USAFIRISHAJI WA SHEHENA ZA MAKONTENA

Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), leo tarehe 13 Mei, 2026 limefanya kikao cha pembeni na viongozi wa Vyama vya Wasafirishaji ikiwemo TATOA na TAMSTOA pamoja na Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA)wakati wa Wasilisho la Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka wa Fedha 2026/2027, Bungeni, jijini Dodoma.

Kikao hicho kiliongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa TASAC, Bw. Mohamed Salum, kilihusisha majadiliano kuhusu changamoto na fursa zilizopo katika usafirishaji wa shehena za makontena na namna ya kuboresha ufanisi wa mnyororo wa ugavi nchini. 

Akizungumza katika kikao hicho, Rais wa TAFFA, Bw. Edward Urio, alisema mawakala wa forodha bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo ucheleweshaji wa malipo na ongezeko la gharama za ucheleweshaji (demurrage).

Kwa upande wake, Mjumbe wa TATOA, Bw. Fahmy Ahmed, alisema chama hicho kiko tayari kusaidia kupunguza msongamano wa mizigo bandarini endapo kitawezeshwa ipasavyo. 

Nae, Mwenyekiti wa TAMSTOA, Bw. Shaban Chuki, alishauri Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kufikiria kujenga barabara za kulipia nchini ili kuondoa changamoto ya foleni. 

Aidha, wadau hao walipongeza kuongezeka kwa mizigo hususan ya mbolea pamoja na juhudi za TASAC katika kuendelea kuratibu na kusimamia sekta ya usafirishaji nchini. Pia, walisisitiza umuhimu wa kutumia ongezeko la mizigo inayokuja nchini kama fursa ya kuimarisha mnyororo mzima wa ugavi. 

Wadau hao pia walijadili changamoto za viwango vya ubadilishaji fedha za kigeni, na gharama za ongezeko la ujazo wa mizigo, na uhaba wa vifaa katika baadhi ya bandari kavu, hali inayochangia ucheleweshaji wa utoaji wa shehena.

Akihitimisha kikao hicho, Bw. Salum alisema sekta ya usafiri kwa njia ya maji inasimamiwa kwa kuzingatia sheria za kimataifa na kwamba Serikali inaendelea kufanya juhudi mbalimbali kuhakikisha shehena zinazokwenda nje ya nchi kuanza  kuchukuliwa kutoka mkoani Morogoro. 

Alitumia fursa hiyo, kushauri TATOA kusaini hati ya makubaliano (MoU) na TASAC ili kurahisisha utendaji kazi na kuimarisha ushirikiano kati ya pande hizo mbili ili kuendeleza sekta ya uchukuzi nchini.

Mrejesho, Malalamiko au Wazo