TASAC YAKUTANA NA WADAU WA UGOMBOAJI NA UONDOSHAJI WA SHEHENA
Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) leo tarehe 14 Januari, 2026 wamekutana na wadau wa ugomboaji na undoshaji wa shehena katika ukumbi wa Chuo cha Utalii jijijini Dar es Salaam.
Akiongea katika kikao hicho Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Bw. Mohamed Salum, ametoa wito kwa wadau wa usafiri majini kushirikiana na TASAC ili kutoa maoni kuhusu kuweka viwango vya chini vya tozo za huduma za ugomboaji na undoshaji wa shehena hatua itakayosaidia kuimarisha na kuboresha huduma.
Lengo la kikao hicho ni kupokea maoni kuhusu uwekaji wa viwango vya chini vya tozo katika huduma za uwakala wa forodha nchini.
“Kwa nyakati tofauti, TASAC imekuwa ikipokea maombi kutoka kwa wadau wakitaka, TASAC iweke viwango vya chini vya tozo katika huduma za ugomboaji. Leo mmepata jukwaa rasmi la kujadili na kutoa maoni yenu kwa uwazi na uhuru ili kufikia mwafaka wa pamoja,” amesema Bw. Salum.
Kwa upande wa Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA), Bw. Edward Urio, pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Bandari Kavu, Bw. Meleck Shange, wameipongeza TASAC kwa kuanzisha mchakato huo wakisema utaongeza uhai wa kampuni za uwakala wa forodha, kudhibiti ushindani usio wa haki na kupanua wigo wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
Mchakato huo wa ukusanyaji wa maoni ni sehemu ya utekelezaji wa Kifungu cha 29 cha Sheria ya Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania, Sura ya 415, kinachoitaka TASAC kukusanya maoni ya wadau kabla ya kufanya maamuzi kuhusu tozo au viwango vya huduma.
TASAC imewahimiza wadau kuendelea kuwasilisha maoni yao kwa maandishi hadi tarehe 20 Januari, 2026, kupitia barua pepe tariff@tasac.go.tz